WAZIRI wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) ameiagiza Bodi ya Wakurugenzi ya Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB), kukuza juhudi za Serikali za kurasimisha mifumo ya masoko kwa lengo la kupunguza vipingamizi vinavyozuia uzalishaji wenye tija.
Mhe. Dkt. Kijaji ameitaka bodi hiyo kutafuta masoko ya bidhaa mbalimbali hususan mazao ya kilimo ili kuongeza tija kwa wakulima.
Waziri Dkt. Kijaji ameyasema hayo Leo tar. 28 Oktoba, 2022 jijini Dar es Salaam, wakati wa Uzinduzi wa Bodi mpya ya WRRB.
“Bodi hii wajumbe wake nawaamini sana na nnajua mtafanya kazi Kwa bidii katika kutatua kero mbalimbali hasa gharama zinazohusika na masuala ya wafanyabiashara wa bidhaa na wakulima wakati wa kufanya biashara,” Amesema Dkt. Kijaji.
Mhe. Dkt. Kijaji amewataka wajumbe hao kuweka utaratibu wa kupata takwimu za soko na mauzo za kuaminika kwa wadau mbalimbali, ili kuongeza ushiriki wa wafanyabiashara wa bidhaa za wenyeji katika biashara ya kimataifa.
Dkt. Kijaji aliitaka bodi kuhimiza usindikaji wa mazao ya msingi nchini, kwa lengo la kuongeza thamani na kukuza uendelezaji wa viwanda.
“Kuongeza upatikanaji wa sehemu zilizo bora za kuhifadhia mazao, kupunguza hasara za baada ya kuvuna na kuimarisha uhakika wa chakula na kuongeza wigo wa wananchi kukopa katika asasi za fedha kwa kutumia mazao yao kama dhamana“, Alisema.
Mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi ya WRRB Prof. Geraldine A. Rashely Amesema kuwa wajumbe wote watafanya kazi Kwa kujiamini Kwa maslahi mapana ya Nchi yetu.
Prof. Rashely kaongeza kuwa bodi ya WRRB itafanyia kazi pia changamoto zinazowakabili watumishi ili wafanye kazi kwa bidii katika kuwahudumia wananchi.