Home Burudani BODI YA FILAMU YAWAITA WASANII KUWASILISHA KAZI ZAO KUWANIA TUZO DESEMBA...

BODI YA FILAMU YAWAITA WASANII KUWASILISHA KAZI ZAO KUWANIA TUZO DESEMBA 2022 ARUSHA.

NA BONIFACE GIDEON, TANGA

Bodi ya Filamu Tanzania leo mkoani Tanga imeanza zoezi la ukusanyaji wa kazi za sanaa za wasanii wa filamu mbalimbali hapa nchini kwaajili ya kuzishindanisha kwenye kinyang’anyiro cha kushindania tuzo za filamu kwa mwaka huu wa 2022 Zitakazofanyika mwezi Desemba huko mkoani Arusha.

Akizungumza meneja mipango na masoko kutoka Bodi ya filamu Tanzania Goodluck Chuwa amewataka Wasanii wa Filamu hususani wa Mkoa wa Tanga kujitokeza kwa Wingi kuwania tuzo hizo nakwamba kazi zote zinatakiwa kuwasilishwa katika Ofisi za Ofisa Utamaduni Mkoa huo wa Tanga hii ni kwa Mkoa wa Tanga lakini pia Ofisi Bodi hiyo Jijini Dar esSalaam salaam .

Alisema kuwa wanaendelea kuunga mkono juhudi za serikali kuzidi kuitangaza Tanzania kupitia filamu ikienda sambamba na uzinduzi wa Royal Tour ambayo ilizinduliwa mwaka 2021 na Rais Samia.

Meneja huyo alisema zoezi hilo la ukusanyaji wa filamu ambalo limezinduliwa leo mkoani Tanga litaendelea hadi Oktoba 30 ambapo kazi za wasanii kutoka mikoa zaidi ya 18 zitakusanywa zikishindanishwa katika vipengele 31.

“Mkoa wa Tanga umekuwa wa kwanza kabisa katika kukusanya filamu hizi lengo ni kuhakikisha wasanii wa sekta ya filamu wanaendelea kunufaika katika Mapinduzi makubwa ambayo yanafanywa na serikali , tutakumbuka Mheshimiwa Raisi alifanya filamu ya Royal Tour hii ni kama taa inayotuambia kuwa sekta ya filamu inakwenda kubadilika sio tu kwenda kupata Umaarufu lakini sasa hivi filamu ni biashara na uchumi , filamu ni kazi, tutapita zaidi ya mikoa 18 ya Tanzania bara na mwisho wa mwezi huu itakuwa ni mwisho wa kupokea filamu zote” alisema Goodluck.

Aidha ameipongeza serikali kwa kuanzisha mashindano hayo ya filamu ambayo yameleta mapinduzi makubwa na kuinua ari na hamasa kwa wasanii mbalimbali hapa nchini ambapo sasa kazi zao zinaonekana na kuingia kwenye masoko ya kiushindani hadi nje ya nchi.

“Tulikuwa hatuna tuzo za filamu lakini bodi ya filamu ilianzisha mchakato huu ambao mpaka sasa umeleta mafanikio makubwa tumeshuhudia wenzetu sasa hivi kupitia sekta hii wameanza kunufaika tumeanza kuona washindi kwenye shindano la kwanza la mwaka jana lililofanywa na serikali na Slsasa hivi tunaona filamu nyingi zinaingia kwenye masoko ya kimataifa” alisema

Kwa upande wake Ofisa Utamaduni wa Mkoa wa Tanga Emmanuel Makene amewataka wasanii wa filamu kuendelea kupelekea kazi zao nyingi zitakazoingia kwenye ushindani na mikoa mingine na hatimaye kuufanya mkoa huo kuibuka na ushindi.

“Tumefarijika sana na ujio wa bodi ya filamu Tanzania tutaendelea kukusanya kazi zote za wasanii ambao wanatakiwa wazifikishe kwenye ofisi ya mkoa ya utamaduni lakini msanii kama unaweza kwenda katika ofisi za makao makuu ya bodi ya filamu ukaziwasilisha wewe mwenyewe, rai yangu wasanii wajitokeze mapema ili mchakato huu ufanyike mapema kwa uhakika zaidi” alisema Makene.

Mwenyekiti wa chama cha waigizaji Mkoa wa Tanga Mohammed Amri Majuto na mkurugenzi wa Majuto Sanaa group alisema amewataka wasanii kutumia fursa ya filamu kujiingizia kipato akiwataka wanatanga kuwapigia kura katika kinyang’anyiro hicho.

Tunashukuru bodi ya filamu kutuletea fursa hii mkoa wa Tanga tupende sana kuzitumia kwa sababu zikishaondoka tutakuja kuzijutia na wasanii hii ni nafasi yao kujitambulisha nina uhakika kwa filamu tulizoziandaa tutashinda katika vipengele mbalimbali tumejipanga vizuri na tumeandaa filamu za kiushindani” alisema Majuto.

Baadhi ya wasanii waliokabidhi filamu zao akiwemo Haroun Mchuzi na Nasra Juma wameipongez bodi ya filamu kwa jitihada inazoendelea kuzifanya kuinua tasnia ya Filamu hapa nchini huku wakieleza matumaini yao ya ushindi kwa kazi ambazo wameziwasilisha na kuwataka wananchi wa mkoa wa Tanga pamoja na wadau wa filamu kujitokeza kuwaunga mkono.

Mwisho

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!