Na Raphael Kilapilo
Wananchi Mkoani Mbeya wanatarajia kunufaika na kiasi cha shilingi bilioni 18.2, pesa zilizotengwa kutekeleza miradi mbalimbali ya barabara na madaraja.
Mhandisi Florian Kabaka, ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA), amebainisha hayo wakati wa ukaguzi wa Daraja la Mwasanga linalounganisha kata za Mwakibete na Tembela, Halmashauri ya Jiji la Mbeya.
“Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia kutoa kiasi cha fedha hizo bilioni 18.2 zinazoenda kuwanufaisha wananchi wa Mbeya,” alisema Mhandisi Kabaka.
Alieleza kuwa pamoja na ujenzi wa Daraja la Mwasanga litakalogharimu kiasi cha shilingi 1,985,044,200, fedha hizo zitajenga kwa kiwango cha lami barabara za Inyala-Simambwe (km 16.7) shilingi 7,052,878,707; Lupeta-Izumbwe (km 10) shilingi 4,516,401,000; Masebe-Lutete(km 7.2) shilingi 2,577,042,388; na Masebe-Bugoba kibaoni (km 5) shilingi 2,123,900,000.
“Wananchi wafahamu wazi kuwa fedha hizi zipo tayari zimeisha kasimiwa na siyo zakutafuta. Sasa ni kazi ya wakandarasi kuongeza kasi ya ujenzi ili miradi ikamilike kwa wakati na kuleta manufaa kwa wananchi,” alisema Mhandisi Kabaka.
Aidha mhandisi Kabaka aliagiza watendaji kuongeza usimamizi na kulipa wakandarasi kwa wakati ili kusiwe na kisingizio chochote, kwa kuwa fedha zipo.
Kwa upande mwingine ndugu Maonyeshwe Mbwiga mkazi wa Mwakibete aliishukuru Serikali kwa kuwajengea daraja litakalo waondolea kero walizokuwa wakipata.
“Hili daraja mwaka juzi lilibomolewa na mvua na kuna watu wawili walipoteza maisha, mbunge wetu Mhe. Tulia Akson alikuja hapa na kuahidi kuwa daraja jipya litajengwa. Sasa tunaona kweli mafundi wapo wanaendelea na ujenzi, hata sisi wananchi tunaona kweli Serikali inafanya kazi, tunashukuru sana,” alisema Mbwiga.
Naye Aron Nyembele, mwanafunzi wa Sekondari Mwakibete alisema kuwa walikuwa wanapata shida kuvuka baada ya daraja kubomoka na wamefurahi kuona daraja jipya na la kisasa linajengwa.
“Tunashukuru kuona daraja hili linajengwa sasa tutapita kwa amani bila wasiwasi wowote. Tunamshukuru sana Rais wetu Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kutujali,” alisema Nyembele.
Bodi ya Ushauri TARURA inaendelea na ziara ya kikazi mkoani Mbeya kukagua miradi mbalimbali inayoendelea kutekelezwa na iliyo kamilika ili kuhakikisha adhma ya Serikali ya kuboresha na kufungua barabara mpya za Vijijini na Mijini na kuwaletea maendeleo wananchi inatimia.