Home Kitaifa BILIONI 12 KUBORESHA BARABARA ZA TARURA RUKWA

BILIONI 12 KUBORESHA BARABARA ZA TARURA RUKWA

Meneja wa TARURA Mkoa wa Rukwa Mhandisi Samson Kalesi akitoa taarifa kuhusu mikataba itakayosainiwa na wakandarasi ambapo jumla ya mikataba 29 yenye thamani ya shilingi Bilioni Sita imesainiwa leo mjini Sumbawanga.
Mmoja wa wakandarasi wa miradi ya ujenzi wa barabara Bw. George Stephen (kushoto) akisaini mkataba pamoja na Meneja wa TARURA Rukwa Mhandisi Samson Kalesi (kulia) leo mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Queen Sendiga Ieo mjini Sumbawanga.
Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Bw. Rashid Mchatta akizungumza kwenye halfa ya utiaji saini mikataba ya ujenzi wa barabara chini ya TARURA leo mjini Sumbawanga ambapo amesema atashirikiana na watendaji wengine wa serikali kufanya usimamizi wa karibu wa miradi hiyo.

Na. OMM Rukwa

Serikali ya Awamu ya Sita imeupatia mkoa wa Rukwa shilingi Bilioni 12 kwa ajili ya ujenzi na matengenezo ya barabara chini ya Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) kwa mwaka wa fedha 2022/2023.

Akizungumza kwenye hafla ya utiaji saini mikataba 29 ya ujenzi na matengenezo ya barabara kati ya TARURA na wakandarasi leo (07.09.2022) mjini Sumbawanga Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Queen Sendiga alisema fedha zilitolewa  zinatokana na mfuko wa barabara na tozo ya mafuta.

Sendiga aliwataka wakandarasi hao kwenda kutekeleza mikataba ya ujenzi na ukarabati wa barabara za vijijini na mitaani kwa weledi na ubora wakizingatia kuwa fedha za watanzania ndizo zinatekeleza miradi hiyo.

Tuna fedha shilingi Bilioni 12 zimetengwa kwenye bajeti ya mwaka 2022/23 kati hizo Bilioni Tano zimetokana na tozo ya mafuta kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa barabara hizi. Sasa lazima tukazifanyie kazi ili wananchi wapate manufaa ”alisema Sendiga.

Mkuu huyo wa Mkoa alitoa agizo kwa wakandarasi kuhakikisha miradi hiyo inakamilika ndani ya miezi sita ya mkataba na kuwa hatopenda kusikia mkandarasi akiomba nyongeza ya muda wa kukamilisha mradi.

Akitoa taarifa kwenye hafla hiyo, Meneja wa TARURA Rukwa Mhandisi Samson Kalesi alisema jumla ya mikataba 29 yenye thamani ya shilingi Bilioni Sita  kwa awamu ya kwanza imesainiwa kwa ajili ya ujenzi na matengenezo ya barabara kwenye halmashauri nne za Rukwa.

Mhandisi Kalesi alitaja shughuli zitakazofanyika kuwa ni ujenzi wa barabara mpya za lami (km 0.5) zitajengwa Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga, (km 1.5) zitajengwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo.

Aidha Mhadisi Kalesi aliongeza kusema kuwa (km 265.95) zitajengwa kwa kiwango cha Changarawe, (km 140.01) zitafanyiwa matengenezo ya maeneo korofi , (km 220.22) zitafanyiwa matengenezo ya kawaida na makaravati 67 na madaraja matatu yatejengwa.

Leo tunashuhudia utiaji saini wa mikataba  29 kati ya TARURA na wakandarasi yenye jumla ya Shilingi 6,182,956,557.60kwa ajili ya kutekeleza kazi mbalimbali za ujenzi na matengenezo ya barabara, madaraja na makalavati, mikataba hii ni ya awamu ya kwanza ambayo ni sawa na asalimia 60% ya kazi zote zitakazo tekelezwa kwa mwaka wa fedha 2022/2023” alisema Mhandisi Kalesi.

Kwa upande wake mwakilishi wa wakandarasi mkoa wa Rukwa Gaudence Kipesha alisema wanaipongeza TARURA kwa kuandaa mikataba inayoeleweka na yenye uwazi tofauti na miaka ya nyuma na kuwa wataenda kuitekeleza kwa ubora na kuzingatia muda uliokubalika .

TARURA Mkoa wa Rukwa inahudumia barabara za lami zenye urefu wa kilometa 41.817, changarawe zenye urefu wa kilometa 847.18 na barabara za vumbi zenye urefu wa kilometa 1418.66

Mwisho.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!