Na. Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Kampuni ya michezo ya kubashiri nchini Tanzania, Betika imezindua Kampeni ya Sodo 4 Climate, Kampeni ambayo inahamasisha utunzaji wa Mazingira kupitia mchezo wa Sodo yenye Kaulimbiu ‘Shabikia Soka sio uharibifu wa Mazingira.’
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Kampeni hiyo, Meneja Mkuu wa Betika, Tumaini Maligana amesema lengo ni kupambana na kupunguza mabadiliko ya tabia nchi kwa ujumla kupitia utunzaji wa Mazingira sanjari na kuhakikisha hali ya hewa inakuwa nzuri, na jamii inakuwa na afya bora.
Katika Kampeni hiyo ya Sodo 4 Climate kutakuwa na Ligi kwenye mchezo wa Soka la Ufukweni katika viwanja vya Coco Beach, Dar es Salaam ambapo Betika wamealika jumla ya timu nane huku Ligi hiyo ikichezwa ndani ya wiki saba.
“Ligi hii itahusisha timu zifuatazo, Betika Staff FC, Coco Beach FC, Espanyol FC, Bodaboda Msasani FC, IPP Media, pia kila timu itakuwa na timu za wanaume na wanawake ambapo kila Jumamosi kutakuwa na mechi moja ya wanaume na mechi moja ya wanawake,” amesema Maligana
Maligana amesema katika wiki saba za Ligi hiyo kutakuwa na matukio mbalimbali ya utunzaji wa mazingira na maendeleo ya jamii kwa ujumla. Mwisho wa mashindano hayo Washindi watapata zawadi.
Hata hivyo, ufunguzi wa Kampeni hiyo ya Sodo 4 Climate ulitanguliwa na shughuli ya usafi wa mazingira na kutoa elimu kuhusiana na masuala ya usafi kwa ujumla sanjari na kuhifadhi taka katika maeneo husika.
Mchezo wa ufunguzi, timu ya Betika Staff FC ilichapwa mabao 3-1 na timu ya Coco Beach FC katika viwanja hivyo vya Coco Beach, Dar es Salaam.