Barabara ya Kimara -Bonyokwa -Kinyerezi inayounganisha Jimbo la Ubungo na Jimbo la Segerea imekabidhiwa kwa Mkandarasi tayari kwa kuanza kujengwa.
Barabara hiyo yenye urefu wa Km 6 inayojengwa kwa kiwango cha lami imekabidhiwa rasmi Machi 09, 2024 na Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila kwa Mkandarasi wa Kampuni ya Nyanza.
Akizungumza na wananchi katika makabidhiano hayo Mbunge wa Jimbo la Ubungo Prof. Kitila Mkumbo amesema kwa muda mrefu Wananchi wamekuwa na shauku ya barabara hiyo ambayo imekuwa kero kwao hasa nyakati za mvua.
Prof. Kitila Mkumbo amesema kwa nyakati tofauti kwa kushirikiana na Mbunge wa Jimbo la Segerea Bona Kamoli wamekuwa wakifuatilia ujenzi wa barabara hiyo ndani na nje ya Bunge.
Prof. Kitila amesema miongoni mwa ahadi zake kubwa kwenye Jimbo la Ubungo ni barabara hiyo iliyopo katika Kata ya Kimara hivyo kwa kujengwa kwake tayari ahadi yake imetimia.
“Katika kampeni mwaka 2020 niliahidi kujenga Barabara hii na ile ya Suka Golani ambayo nayo imeshaanza kujengwa, zipo nyakati za kununiwa, kucheka na kupiga makofi, Sasa huu ni wakati wa kicheko kwa watu wa Mavurunza” Prof. Kitila Mkumbo.
Akikabidhi barabara hiyo mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila ameonya Wananchi wenye mpango wa kwenda Mahakamani kuzuia ujenzi huo kuwa wanarudhisha nyuma maendeleo.
“Zipo barabara zilizoshindwa kujengwa kwa kisingizio kuwa zinapita kwenye makazi ya watu waliokwenda kufungua kesi Hela zikapelekwa mahala pengine, Sasa msifanye hivyo na hapa, Iwapo mtafungua kesi mkashindwa tutabomoa mara moja bila kujali ndani kuna nini” Albert Chalamila Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Miradi TANROADS Japherson Nnko akiwa katika hafla ya kukabidhi mradi wa unjenzi wa barabara ya Kimara – Bonyokwa – Kinyerezi amesema ujenzi wa barabara hiyo utakamilika Julai 2025 .
Nnko amesema barabara hiyo ina urefu wa Km 6 na mapana mita 14 zikijumuisha barabara, taa za barabarani, mitaro itakayofunikwa sehemu zenye watu wengi na njia za waenda Kwa miguu huku kukiwa na Daraja moja lenye urefu wa mita 20.
Mkandarasi wa Nyanza Roads Works aliyekabidhiwa barabara hiyo, ameahidi kuijenga Kwa kiwango na Kwa wakati uliopangwa.
Mwisho