Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) Mkoa wa Mtwara imepokea Mitambo miwili ya kupakia na kushusha mizigo (mobile hubour crane) kutoka Bandari za Dar es Salaam na Tanga.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania TPA makao makuu Nicodemus Mushi, ambae ni Meneja Uhusiano na Mawasiliano kutoka makao makuu ya TPA leo machi 12,2024 amesema kuletwa kwa vifaa hivyo ni utekelezwaji wa agizo la Mhe,Rais Samia Suluhu Hassan ambapo aliagiza kuletwa kwa vifaa ili kazi iweze kufanyika kwa ufanisi zaidi.
“Kabla ya uwekezaji uliofanyika hapa uwezo wa bandari hii ilikuwa ni kuhudumia meli na shehena takribani tani laki 4 kwa mwaka,baada ya uwekezaji uwezo umeongezeka hadi kufikia zaidi ya tani milioni 1 kwa mwaka.”
“hivyo uwekezaji huo ulihitaji vifaa ili kazi iweze kufanyika na sisi tunatekeleza.”Amesema Mushi.
Naye Mhandishi Humphrey Kiwia amesema Mitambo hiyo miwili iliyofika kwenye bandari hiyo mmoja unauwezo wa kuhudumia tani 100 na mwengine tani 63 na kufanya bandari ya mtwara kuwa na mitambo mitatu ambayo itauhudumia mizigo mbalimbali kama makasha.
Dunstan Kazibure akiongea kwa niaba ya Meneja wa bandari ya Mtwara,ameongeza kuwa kabla ya kufika kwa mitambo hiyo miwili utendaji kazi ulikuwa wa kusuasua kutokana na kuwepo kwa kifaa kimoja hali iliyokuwa inasababisha kuzidiwa kwa kazi.
“Awali changamoto moja wapo ilikuwa ni kuwa na kifaa kimoja ambacho kilikuwa kinahudumia meli ndogo ndogo na baadhi ya meli kubwa za kubebea makaa na wakati mwengine kifaa hicho kilikuwa kinatumika kwenye maeneo mengine na wakati mwengine kilikuwa kinahabika hivyo ujio wa vifaa hivi tunaamini itaondoa changamoto tuliyokuwa nayo.”Amesema Kazibure