Home Kitaifa BABA NA MAMA LISHE DODOMA MJINI WAPATIWA BURE MITUNGI YA GESI YA...

BABA NA MAMA LISHE DODOMA MJINI WAPATIWA BURE MITUNGI YA GESI YA ORYX 500 NA MAJIKO YAKE

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

KAMPUNI ya Oryx Gas kwa kushirikiana na Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini ambaye pia ni Waziri wa Madini wamegawa bure mitungi ya gesi 500 pamoja na majiko yake kwa Baba na Mama Lishe wa Jimbo hilo kwa lengo la kuwawezesha kurahisha shughuli zao za kuandaa chakula sambamba na kulinda afya zao.

Akizungumza leo Julai 13,2024 wakati wa kugawa mitungi hiyo, Mkurugenzi wa Oryx Gas Tanzania Benoite Araman amesema mitungi hiyo 500 ya gesi ya oryx na majiko yake yamegharimu Sh.milioni 41 na kwamba wataendeela kufuata maelekezo ya serikali inayoongozwa na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan inayohamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kuendeela kugawa mitungi hiyo kwa wananchi wa makundi mbalimbali.

Amesema Oryx Gas wanaamini kupika kwa gesi kunalinda mazingira kwa kuacha kukata kuni na mkaa lakini inalinda afya kwa kuwaepusha kuvuta moshi na mvuke unaoathiri mapafu na afya yao unaotokana na kuni na mkaa hivyo Baba na Mama Lishe ni kundi ambalo wanalipa kipaumbele kwa kutambua ndilo linatumia zaidi kuni na mkaa kila siku kwa shughuli zao za kuandaa chakula.

Pia amesema kwa kutumia nishati safi ya kupikia inayotokana na gesi wanawake wanatumia muda mchache kupika, hivyo wanapata nafasi kufanya shughuli nyingine za maendeleo na kuepuka kugombana na wenza wao kwa kuchelewesha chakula.

“Katika ngazi ya familia tunafahamu kuna watoto ambao wamekuwa wakienda kutafuta kuni na hivyo kutumia muda mwingi kusaka kuni na kukosa muda wa kutosha wa kusoma na kwenda darasani, hivyo kutumia gesi kutasaidia watoto kupata muda wa kusoma na kulinda afya zao.Kwa miaka mingi Oryx Gas tumekuwa kiongozi katika kukuza matumizi ya gesi nchini.

“Kuanzia Julai mwaka 2021 tumekuwa mstari wa mbele kutekeleza maelekezo ya Serikali tulioyapokea kutoka kwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kuwa ifikapo mwaka 2023 asilimia 80 ya wananchi watumie nishati safi ya kupikia,” amesema na kusisitiza kupitia mipango hiyo, Oryx Gas inataka kutokomeza matumizi ya nishati chafu ya kuni na mkaa.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Athony Mavunde amesema wanashukuru kwa kupata majiko hayo huku akieleza na wao wamejipanga vizuri kuhakikisha wanaenzi kampeni ya kutunza mazingira hasa kwa kuwa na mipango mbalimbali ili wananchi wengi wasitumie nishati ya kuni na mkaa ambayo kwa kiwango kikubwa inaharibu mazingira.

Amesisitiza anaishukuru anawashukuru Kampuni ya Oryx chini ya uongozi wa Araman Benoite kwa kukubali ombi lao la kuwashika mkono Baba na Mama Lishe wa Dodoma Mjini kwa kuwapatia majiko ya gesi na majiko yake , hivyo kazi yao kubwa ni kuhakikisha wanalinda mazingira.

“Pia nichukue fursa hii kumshukuru Rais Dk.Samia Samia Suluhu Hassan ambaye yeye ndio muasisi wa utunzaji mazingira kwa kutumia nishati safi na alitoa maelekezo kwamba ifikapo mwaka 2032 basi asilimia 80 ya wananchi wawe wanatumia nishati safi ili kuondokana na uchafuzi wa mazingira ambao umesababisha mabadiliko ya tabianchi kwa kiwango kiwango kikubwa.

“Tunamshuku Rais Samia kwa kuweka kipaumbele na kuwa kidede kusimamia jambo hili na kama mnavyoweza kuona mitingu ambayo imetolewa hapa itapunguza matumizi ya mkaa na tukipunguza matumizi ya kuni na mkaa tututakuwa tumepunguza uharibifu wa mazingira pamoja na kulinda afya zetu kwani tunatambua watumiaji wa kuni na mkaa wamekuwa wakipata madhara ya kiafya kwa kuvuta moshi na hasa baba na mama lishe.”

Amesema kampeni ya Rais Samia kuhamasisha nishati safi inakwenda kuokoa maisha ya baba na mama lishe ambao kwa sehemu kubwa muda wao mwingi unatumika kupika na wengi wao wanatumia kuni na mkaa, hivyo kupitia nishati hiyo wanakwenda kuepukana na madhara ya kiafya yanayotokana na matumizi ya kuni na mkaa.

Wakati huo huo Mbunge wa Viti Maalum Tanzania Bara anayewakilisha kundi la Asasi za Kiraia kupitia Chama Cha Mapinduzi(CCM) Neeema Lugangira amesema anaelewa changamoto ambazo wanawake wanazipitia katika kuandaa chakula nyumbani.

“Kunachangamoto za akina mama kutumia muda mwingi kwenda kutafuta kuni , watoto wanatumia muda mwingi kwenda kutafuta kuni.Kuna kadhia nyingi ambazo tunazipitia wakati wa kwenda kutafuta kuni ikiwemo ukatili wa kijinsia , muda mwingi tunaotumia kutafuta kuni muda ule tungeweza kufanya shughuli nyingine za kiuchumi.

“Kwahiyo Rais Dk.Samia Suluhu Hassan alipokuja na ajenda ya kutafuta nishati safi na salama ya kupikia moja ni kuokoa afya zetu kwani akina mama na watoto wanapata madhara makubwa kutokana na moshi ule ambao tunavuta wakati wa kupika,”amesema.

Awali Mkuu wa wilaya ya Dodoma Mjini Alhaj Jabiri Shekimweri amepomngeza Waziri Mavunde kwa jinsi anavyojitoa kwa ajili ya wananchi wa Jimbo la

Dodoma Mjini wakiwemo Baba na Mama Lishe huku akitumia nafasi hiyo kusisitiza ni vema walipewa mitungi ya gesi na majiko yake kuhakikisha wanaitumia vema gesi hiyo ili wasipate madhara.

“Nitoe rai kwa wote ambao wamepatiwa gesi hii,kabla ya kuitumia wapate elimu kuhusu namna nzuri ya kutumia gesi bila kupata madhara.Nimefurahi kusikia Oryx pamoja na kutoa mitungi hii wameamua kutoa na elimu kuhusu matumizi sahihi ya mtungi wa gesi.”

Mwisho

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!