Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amezindua Bodi za Mamlaka za Maji Nchini na kuwataka viongozi wa Sekta ya Maji kuhakikisha wanashirikiana na wadau wengine katika kuhakikisha Sekta ya Maji inasonga mbele kwa kuishirikisha jamii katika hatua mbalimbali za kufanikisha huduma ya maji.
Waziri Aweso amesema hayo akifungua kikao cha mafunzo kwa Wakurugenzi na Menejimenti za mamlaka za majisafi na usafi wa mazingira, jijini Dar es salaam ambapo amemtaka Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Prof. Jamal Katundu kuhakikisha bodi hizo zinakuwa mkono wa wizara na kupokea maoni mbalimbali kutoa majibu kutoka kwa makundi mbalimbali wakiwemo viongozi wa kisiasa, viongozi wa Serikali, wafanyabiashara na watumishi wastaafu waliobobea katika masuala ya maji.
“Hatuwezi kufanya kazi peke yetu. Lazima tuhakikishe tunashirikiana na wadau wengine ili kuhakikisha tunafikia malengo tuliyojiwekea” Mhe. Aweso amesema na kuongeza lengo ni kufika upatikanaji wa huduma yam aji vijijini kwa asilimia 85 na mijini asilimia 95, na kupita kiwango hicho ili kuwafikia wananchi na “kumtua mama ndoo ya Maji kichwani”.
Amesema hivi sasa zoezi la utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maji linaendelea vizuri na jambo la kuangalia ni kuhakikisha utoaji wa huduma za uhakika na taarifa kwa wateja pale inapotokea hitililafu katika uzalishaji wa maji. Akizungumzia suala la upotevu wa maji (NRW) amezitaka bodi kufuatilia kwa kina kuhusu mivujo na kiwango cha maji kinachopotea ili kuona uhalisia wa maji taarifa kwasababu inawezekana maji yanatumika bila kulipiwa.
Mafunzo hayo yameshuhudia bodi za wakurugenzi za mamlaka za maji 25 zikizinduliwa na baadhi ya mamlaka za maji zikipandishwa madaraja kuendana na vigezo ikiwamo vya utoaji huduma na kumudu kujiendesha.