NA.MWANDISHI WETU
Askofu Mkuu wa Kanisa la E.A.G.T nchini Dkt. Brown Abel Mwakipesile amewaasa washirika wa kanisa hilo kushiriki kikamilifu katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi linalotarajiwa kufanyika Agosti 23, 2022 kwa kuzingatia umuhimu wa zoezi hilo katika maendeleo ya nchi yetu.
Askofu Mwakipele ametoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuhitimisha ibada maalum ya kumaliza mkutano mkubwa wa injili wa kanisa hilo tarehe 7 Agosti, 2022 katika kanisa lake lililopo Maili Mbili Jijini Dodoma.
Alisema, kila muumini anawajibika kushiriki katika Sensa ya Watu na Makazi kwa kuzingatia umuhimu wake, katika mipago mbalimbali ya maendeleao ya nchi.
“Kila mmoja aone umuhimu wa kushiriki katika zoezi hili, ili kusaidia Serikali yetu katika kurahisisha mipango ya maendeleo iliyopo kufanikiwa,”Alisema Dkt. Mwakipesile
Aliongezea kuwa, wataendelea kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan kwa maendeleo anayoyafanya katika nyanja mbalimbali ikiwepo kuitangaza nchi kimataifa.
Aidha ,Askofu Dkt. Mwakipesile ametoa shukrani pamoja na pongezi kwa serikalii kwa namna inavyotoa nafasi na vibali katika kuhubiri injili ambayo ndiyo lengo la kanisa hilo ili kila mtu afikiwe na injili na kuacha dhambi na kutenda mambo mema.
”Naishukuru sana Nchi yetu kwa vile ambavyo imetoa uhuru wa kwamba neno la Mungu lihubiriwe kwa watu wote katika Nchi yetu kwa sababu neno la Mungu ndio Baraka na Ufunguo pekee katika Maisha ya Mwanadamu” alisisitiza askofu Mwakipesile.
Hata hivyo Askofu Mwakipesile amebainisha kuwa katika mkutano uliokuwa ukifanyika kanisani hapo kwa muda wa siku 8 umekuwa wa baraka na miujiza mkubwa imetendeka ikiwemo watu kufunguliwa katika mateso mbalimnbali ikiwemo magonjwa na watu wengi kufunguliwa vifungo vilivyokuwa vinatesa maisha yao.
=MWISHO=