Asasi za kiraia nchini, kupitia Shirika la The Foundation for Civil Society (FCS), zimesisitiza umuhimu wa Serikali kuwezesha makundi maalum kufikia miundombinu ya kidigitali ili kushiriki kikamilifu katika michakato ya maendeleo na kujiimarisha kiuchumi.
Akizungumza katika mkutano wa kitaifa wa watu wenye ulemavu, madiwani, na wadau, uliofanyika Agosti 12, 2024, jijini Dar es Salaam, Meneja Programu wa FCS, Bi. Nasim Losai, alisema kuwa mkutano huo ulilenga kuangazia ushiriki wa watu wenye ulemavu katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Pia, mkutano ulijadili matumizi ya takwimu za sensa katika kuboresha mipango ya halmashauri za wilaya na ngazi za kata.
Bi. Losai alieleza kuwa Serikali imekuwa sikivu katika kuhakikisha makundi maalum yanawezeshwa kushiriki katika shughuli za kiuchumi na kuongeza kipato chao. Alisisitiza kuwa FCS imekuwa ikiunga mkono juhudi hizo kwa zaidi ya miaka 20 ya kufanya kazi na jamii.
“FCS tuna zaidi ya miaka 20 tukisaidia serikali katika shughuli za jamii na kutetea haki za watu wenye ulemavu. Kazi kubwa imefanywa, hususan kwenye kuboresha miundombinu ya majengo kwa kushirikiana na makundi haya,” alisema Bi. Losai.
Mshauri wa kitaalamu wa masuala ya watu wenye ulemavu Tanzania, Peter Charles, aliongeza kuwa mkutano huo uliwaleta pamoja zaidi ya watu 600 wenye ulemavu kutoka Dar es Salaam, wakiwemo madiwani 60 wa viti maalum na wale walioteuliwa. Lengo kuu la mkutano lilikuwa kuwajengea uelewa watu wenye ulemavu kuhusu fursa za kiuchumi na kuhakikisha wanashirikishwa kikamilifu.
“Ushirikishwaji wa watu wenye ulemavu bado ni mdogo, ndiyo maana tumewaalika madiwani ili kujadili changamoto zilizopo na kuhakikisha zinajumuishwa kwenye mipango ya maendeleo ya mabaraza yao ndani ya halmashauri,” alisema Peter Charles.
Mwenyekiti wa Chama cha Walemavu Tanzania, Hamadi Abdallah Komboza, alibainisha changamoto kubwa kwa watu wenye ulemavu kuwa ni ukosefu wa ajira. Aliiomba Serikali, kupitia Kamishna wa Kazi na vyama vya watu wenye ulemavu, kufanya ukaguzi katika mashirika na taasisi zinazopaswa kuajiri watu wenye ulemavu lakini bado hazijatekeleza wajibu huo, akisema msukumo zaidi unahitajika.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu Tanzania, Jonas Lubalo, aliishukuru taasisi ya Ikupa Trust Fund kwa mchango wake mkubwa na huduma kwa watu wenye ulemavu katika maeneo mbalimbali nchini.