SHIRIKA la Viwango Afrika (ARSO) kwa kushirikiana na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) wamewakutanisha wataalamu wa masuala ya afya kutoka nchi 11 barani Afrika kwaajili ya uandaaji viwango vya huduma za afya ili kuboresha huduma kwenye sekta hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo AprilI 08,2024 Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara, Mhe. Sempeho Manongi amesema wamekutana kwaajili ya kuandaa, kujadili, na kuboresha viwango vya huduma za afya ili kuhakikisha tunalinda afya, mazingira na usalama katika bara la Afrika.
Amesema watumiaji wa viwango vya bidhaa na huduma za afya wana mchango mkubwa katika uchumi wa nchi za bara la Afrika kwani wao ndio wazalishaji na watoa huduma wa bidhaa hizo.
“Duniani kote, shughuli za wazalishaji na watoa huduma zimekuwa kichocheo kikuu cha ukuaji wa uchumi kutokana na kuwa chanzo kikubwa cha ajira. Hivyo usalama wa walaji kupitia matumizi ya viwango itasaidia utambuzi wa bidhaa bora na salama kwa matumizi, na pia itapunguza athari ya matumizi ya bidhaa za huduma za afya sizisokidhi matakwa ya viwango”. Amesema
Aidha amesema kuwa bara la Afrika limeingia katika soko huru la Afrika (Africa free continental Trade) ambapo inalazimu kufanya shughuli za kibiashara kwa pamoja,na viwango vya namna hii ni muhimu kwa maana ya shughuli zote za kiafya na bidhaa zinatakiwa kuwa na viwango sawasawa, ambapo nchi itakabidhiwa cheti ambacho itakitumia kwa nchi za Afrika.
Pamoja na hayo ametoa rai kwa kamati ya kitalaam kuzingatia miongozo yote ya uandaaji viwango ili kupata viwango vinavyotekelezeka na ambavyo vitasaidia bara la Afrika kupata faida za matumizi ya Viwango.
Kwa Upande wake, Mkurugenzi wa Shirika la Viwango Afrika (ARSO), Dkt. Hermogène Nsengimana amesisitiza viwango ambavyo vinaandaliwa viwe vinatekelezeka kwa kushirikiana na wadhibiti wa nchi zetu.
Ameeleza kuwa katika mkutano huo watakuwa na kamati mbalimbali ambazo miongoni mwa kamati hizo ni kamati ya masuala ya dawa na ufamasia, kamati ya dawa za asili za kiafrika ambapo zitajadili mambo mbalimbali kwa lengo la kukuza huduma za afya.
“Tuna kamati za ufundi mbalimbali zaidi 74 ambazo zinajadili huduma za afya na baadhi ya maendeleo muhimu katika bara,ambapo tunazaidi ya nchi 6 ambazo zimepiga hatua katika miundombinu bora ya afya na Tanzania ni moja ya nchi hizo”. Dkt.Nsengimana amesema.
Naye Mkurugenzi wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Dkt,Athuman Ngenya amesema kuwa tunakabiliwa na changamoto nyingi katika sekta ya afya barani Afrika, changamoto ambazo zinaweza kuvuka mipaka ya nchi na kuhusisha masuala ya ubora, usalama, na upatikanaji wa huduma za afya.
“Ni jukumu letu kama wataalamu katika eneo hili kuhakikisha kwamba tunajenga mifumo imara ya viwango ambayo itasaidia kupunguza changamoto hizi na kuimarisha sekta ya afya kwa ujumla”. Amesema Dkt. Ngenya.
Mkurugenzi wa Shirika la Viwango Afrika (ARSO), Dkt. Hermogène Nsengimana akizungumza na wataalamu wa masuala ya afya kutoka nchi 11 barani Afrika wakati wa mkutano maalumu kwaajili ya uandaaji viwango vya huduma za afya ili kuboresha huduma kwenye sekta hiyo ambapo mkutano huo umefanyika leo Aprili 08,2024 Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Dkt,Athuman Ngenya akizungumza na wataalamu wa masuala ya afya kutoka nchi 11 barani Afrika wakati wa mkutano maalumu kwaajili ya uandaaji viwango vya huduma za afya ili kuboresha huduma kwenye sekta hiyo ambapo mkutano huo umefanyika leo Aprili 08,2024 Jijini Dar es Salaam.