Na Magrethy Katengu
JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limemkamata na linamuhoji kwa kina Selemani Agai Gaya (18) mkazi wa Kigamboni, kwa tuhuma za kutoa lugha ya matusi mtandaoni dhidi ya Viongozi wakuu wa Serikali Tanzania kwa kutumia mitandao wa kijamii wa Tiktok.
Mtuhumiwa huyo amekamatwa Julai 29, mwaka huu na wenzake wakitengeneza maudhui za mtandaoni (video) na kuzisambaza kwenye mitandao ya kijamii zenye kuwatukana na kuwafedhehesha viongozi wakuu wa Serikali katika akaunti zao za mtandao wa kijamii.
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es salaam mapema leo Agosti 1 Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es salaam SACP Muliro Jumanne amesema
Jeshi la Polisi linatoa onyo kali kwa mtu au watu wanaotoa lugha za matusi na fedheha kwa Viongozi wa Serikali kwa njia ya mtandao na njia nyingine yoyote.
Amesema Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Mamlaka nyingine za kisheria wamejipanga kuwafuatilia na kuwakamata, kuwahoji kwa kina kuhakikisha wanafikishwa haraka kwenye nyombo vya sheria.
SACP Jumanne amesema mtuhumiwa huyo anatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote kuanzia sasa.
Katika hatua nyingine, SACP Jumanne amesema Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam Julai 31, mwaka huu limewakamata watuhumiwa saba akiwemo Amani Kipolo mkazi wa Vingunguti kwa tuhuma za kumshambulia na kusababishia kifo Hadija Hamisi na kuwajeruhi watu wengine nane (8).
Amesema Watuhumiwa hao wakiwa na wenzao wakiwa kwenye kundi waliwashambulia wananchi mtaani maeneo ya Vingunguti kwa lengo la kulipiza kisasi wakati wakitoka kuzimka mwenzao aliyefahamika kwa jina la Nurdin Bwino.
Aidha, amesema awali marehemu huyo Nurdin Bwino aliuwa kwa kushambuliwa na wananchi alipokuwa na wenzake sita wakiwa na visu na vifaa mbalimbali vya kuvunjia alipojaribu kuvunja nyumba moja usiku wa Julai 30, 2023.
Mwisho