Home Kitaifa ACT-WAZALENDO YAPINGA KAULI YA MKURUGENZI WA TUME HURU YA UCHAGUZI

ACT-WAZALENDO YAPINGA KAULI YA MKURUGENZI WA TUME HURU YA UCHAGUZI

Chama cha ACT Wazalendo kimesema kauli ya Mkurugenzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) Dk. Ramadhan Kailima ya kuhalalisha Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) kusimamia uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2024 inapotosha jamii hivyo haipaswi kupita bila kukosolewa vikali.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na chama hicho juni 14, 2024 kupitia Katibu Mkuu wake Ado Shaibu ambaye ameeleza kuwa kauli Dkt. Kailima ipingwe kwa sababu haina msingi wowote wa kisheria na kimantiki.

Dk. Kailima alitoa kauli hiyo tarehe 13 Juni, 2024 akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uboreshwaji wa daftari la wapigakura unaotarajiwa kufanyika kuanzia mwezi Julai, 2024. Kwenye Mkutano huo Dk. Kailima alisema kuwa INEC haina mamlaka ya kusimamia uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa sababu kifungu cha 10(1)(c) cha Sheria ya Tume Huru ya Uchaguzi kimesema INEC itasimamia uchaguzi huo kwa kuzingatia sheria itayotungwa na Bunge ambayo kwa sasa bado haijatungwa.

Kailima amesema kutokuwepo kwa sheria hiyo kunaikosesha INEC wajibu wa kusimamia uchaguzi huo badala yake unaendelea kusimamiwa na TAMISEMI.

Hata hivyo ACT imeendelea kushikilia msimamo wake kwa kusema kuwa kutotungwa kwa sheria ya kusimamia uchaguzi wa Serikali za Mitaa hakuipi nafasi TAMISEMI kusimamia uchaguzi kwa sababu Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa iliyokuwa inaipa madaraka TAMISEMI kusimamia uchaguzi wa Serikali za Mitaa imefutwa na kifungu cha 67 cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya Mwaka 2024.

Kinachopaswa kufanyika sasa ni Serikali kupeleka Muswada kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa kutunga Sheria itakayosimamia uchaguzi wa Serikali za Mitaa chini ya Tume Huru ya Uchaguzi” Ameeleza Ado Shaibu katika taarifa ya Chama hicho.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!