Home Kitaifa ACT WAZALENDO YAANZA MCHAKATO WA WATIANIA KUGOMBEA NAFASI ZA UCHAGUZI 2025.

ACT WAZALENDO YAANZA MCHAKATO WA WATIANIA KUGOMBEA NAFASI ZA UCHAGUZI 2025.

Chama cha ACT Wazalendo kimefungua rasmi mchakato wa ndani wa wanachama kujitokeza na kutangaza nia ya kugombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025. Mchakato huu ulianzishwa rasmi kuanzia tarehe 15 Januari 2025, kama sehemu ya utekelezaji wa agizo la Halmashauri Kuu ya Chama Taifa.

Akizungumza na waandishi wa habari katika hafla ya uzinduzi wa mchakato huo, Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu, alisisitiza kuwa wanachama watakaotaka kugombea nafasi za Udiwani, Ubunge, na Urais wanapaswa kufuata taratibu maalum za kujisajili na kutangaza nia zao kupitia njia mbalimbali, ikiwa ni pamoja na mazungumzo na waandishi wa habari.

Chama chetu kitaendelea kuhakikisha michakato ya uchaguzi inaendeshwa kwa uwazi na demokrasia, na tunatoa fursa kwa wanachama wote wenye sifa za kugombea nafasi hizi kujitangaza,” alisema Ado Shaibu.

Aliongeza kuwa watiania wote wanahitaji kujipima kwa kuzingatia vigezo vya Chama, ikiwemo maadili, haiba, na uwezo wa kujieleza, pamoja na ushiriki wao katika shughuli za ujenzi wa Chama. Viongozi wa ngazi mbalimbali wameagizwa kuweka utaratibu wa kuwashirikisha watiania katika shughuli za Chama, na pia kufanya usaili kwa wagombea wa Ubunge na Urais.

Mchakato huu wa kugombea nafasi za uongozi ndani ya ACT Wazalendo unatarajiwa kuendelezwa kwa misingi ya uwazi na usawa.

Masuala muhimu ya kuzingatiwa kwenye mchakato huu ni kama ifuatavyo;-

  1. Watiania wanapaswa kujisajili kwenye orodha ya watiania kwenye ngazi husika kwa kujaza fomu maalum kama ifuatavyo;
  • Watiania wa Udiwani na Udiwani wa Viti Maalum ngazi ya Kata;
  • Ubunge na Ubunge wa viti maalum ngazi ya Jimbo; na
  • Watiania wa Urais Ofisi ya Makao Makuu.
  1. Watiania wanaruhusiwa kujitangaza kupitia njia mbalimbali ikiwemo kuzungumza na waandishi wa habari. Idara ya Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma ngazi ya Taifa kwa kushirikiana na viongozi wa Mikoa na Majimbo imeagizwa kuhakikisha kuwa watiania wote wanapata nafasi ya kujitangaza kupitia kurasa za mitandao ya kijamii ya Chama na kuwaunganisha na waandishi wa habari na kusambaza taarifa za watiania hao.
  2. Viongozi wa Mikoa, Majimbo na Kata wameagizwa kuwaruhusu watiania kutumia Ofisi za Kata, Majimbo na Mikoa kutangaza nia zao. Kwa ngazi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, watiania wanaruhusiwa pia kutangaza nia kupitia Ofisi ya Makao Makuu ya Chama.
  3. Watiania wanapaswa kujipima kwa kuzingatia vigezo vya watiania ambavyo vimewekwa na Halmashauri Kuu ya Chama. Vigezo hivyo ni pamoja na kutimiza sifa za kugombea nafasi husika zilizoainishwa na sheria za nchi na Katiba ya ACT Wazalendo Toleo la Mwaka 2024 pamoja na Kanuni za Uchaguzi za Chama.

Sifa nyingine ni kuwa na haiba, maadili, uwezo wa kujieleza na maono yanayoendana na nafasi ambayo mtiania anakusudia kuigombea.

Watiania watapimwa pia kwa ushiriki wao katika ujenzi wa Chama. Viongozi wa ngazi husika wameagizwa kuweka utaratibu wa kuwashirikisha watiania katika shughuli za ujenzi wa Chama katika ngazi husika na kutunza taarifa za ushiriki wao.

  1. Chama kitaweka utaratibu wa kuwasaili (interview) watiania kabla ya taratibu za kikatiba za uteuzi wa wagombea. Taratibu na jopo la usaili (Interview panel) litatangazwa baadaye kwa ngazi za Ubunge na Urais. Usaili huo utakuwa wazi kwa umma kupitia vyombo mbalimbali vya habari.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!