Zaidi ya abiria 500 wanaotumia usafiri wa reli ya Tazara kutoka Makambako mkoani Njombe kuelekea Mkamba wilayani Kilombero wamekwama kwa zaidi ya saa 48 katika eneo la Kijiji cha Lumumwe kata ya Kamwene halmashauri ya Mlimba baada ya sehemu ya reli hiyo kufunikwa na maporomoko ya udongo yaliyosababishwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha mkoani Morogoro.
Baadhi ya abiria waliokwama wakizungumzia tukio hilo wamesema kuwa ni siku ya pili sasa wamekwama katika eneo hilo hivyo wanendelea kupata hasara pamoja kukosa chakula
Tukio hilo limelilazimu Jeshi la Wananchi wa Tanzania kikosi cha Anga Kizuka kufika na kuchukua hatua za haraka kuokoa abiria hao,huku mkuu wa Wilaya Kilombero Wakili Dustan Kyobya akimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuliagiza Jeshi hilo kwaajili ya uokozi kwa kutumia helkopta kwani eneo hilo halifikiki kwa chombo chochote cha moto.
Yalianza kukatika mawasiliano ya barabara ya Ifakara – Mlimba na sasa maporomoko ya udongo yaliyosababishwa na mvua kubwa yaliyokatisha safari ya abiria zaidi ya 500 waliokuwa wakitumia usafiri gari moshi ya Tazara kutoka makambako kuelekea Mkamba wilayani Kilombero.