Na Mercy Maimu
Naibu Waziri wa Uwekezaji Viwanda na Biashara amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa ajili ya watu na mashirika binafsi ambayo yapo tayari kuwekeza nchini ili kuendelea kukuza uchumi wa nchi.
Ameyasema hayo akifungua Maonesho ya Sekta ya Dawa na Huduma za Afya yanayofanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee kuanzia Desemba 14 hadi 16 /2022 jijini Dar es Salaam ambapo wadau mbalimbali wa sekta ya afya kutoka Afrika Mashariki wanashiriki.
Amesema Serikali inaweka mazingira wezeshi kwa ajili ya wawekezaji kujenga viwanda vyao hapa nchini ili kurahisisha uzalishaji na ununuzi wa vifaa tiba kwa matumizi ya ndani ya Nchi.
Aidha Amesema Serikali ya Awamu ya Sita imewezesha upatikanaji wa maeneo ambayo wawekezaji wataweza kuwekeza kwa urahisi na kuzalisha vifaa tiba na kuwasaidia wanunuzi kupata bidhaa kwa wakati.
Ameongeza kuwa Watanzania wanatakiwa kuchangamkia fursa hii ya uwekezaji kwa kuzalisha malighafi ambazo zitatumika katika viwanda hivyo.
Kigahe pia amebainisha kuwa maonyesho hayo yamevutia uwekezaji nchini na yamewezesha kutafuta wadau ambao wameonyesha kushirikiana na Watanzania, kubadilishana uzoefu na teknolojia ya kisasa.
Wakizungumza katika maonesho hayo baadhi ya wadau wa sekta ya afya BERNADETHA LYAMUYA na BENSON MEIKOKI wamesema maonesho hayo yanatoa fursa ya kushuhudia vifaa tiba vya kisasa kutoka mataifa mbalimbali na ni chachu kwa sekta ya afya hapa nchini kujipambanua katika uzalishaji wa vifaa tiba vya kisasa.