Home Biashara DKT. KIRUSWA AWATAKA WACHIMBAJI WADOGO LINDI KUTOJIHUSISHA NA UTOROSHAJI MADINI

DKT. KIRUSWA AWATAKA WACHIMBAJI WADOGO LINDI KUTOJIHUSISHA NA UTOROSHAJI MADINI

Na.Samwel Mtuwa- Ruangwa.

Naibu Waziri wa Madini ameyasema hayo leo Desemba 13 , 2022 katika hafla ya uzinduzi wa mafunzo kwa wachimbaji wadogo wa Mkoa wa Lindi yanayotolewa na GST yanayofanyika Wilaya ya Ruangwa yaliyohudhuriwa na zaidi wachimbaji 400.

Dkt. Kiruswa amewasihi wachimbaji na wafanyabiashara ya madini nchini kutojihusisha na utoroshaji madini kwasababu serikali haitakuwa na huruma hivyo kuwataka wanapopata madini kupeleka kwenye soko la Madini ili kupangiwa tozo stahiki za kikodi.

Akielezea juu ya baadhi ya watu wanaoshikilia leseni kubwa kwa muda mrefu bila kuziendeleza Dkt. Kiruswa amewahakikishia wachimbaji wadogo kuwa Serikali ipo mbioni kukamilisha mchakato wa marekebisho ya sheria ya madini ili kuweka utaratibu wa kisheria wa Serikali kutwaa leseni zinazoisha muda wake na hivyo kurudishwa serikalini.

Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Lindi ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Liwale Bi. Judith Nguli ameipongeza Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) kwa kuamua kuleta mafunzo hayo Mkoa wa Lindi na kuwataka wachimbaji wadogo kujifunza na kubadili mitizamo yao ya utafutaji , uchimbaji na uchenjuaji ili kuongeza uzalishaji madini katika sehemu zao za kazi sambamba na hapo ameipongeza GST kwa kuandaa ramani ya madini ya Mkoa wa Lindi na kuiwasilisha katika Wilaya zote na Mkoa Lindi. Aidha, Bi. Judith ameiomba Wizara ya Madini kuangalia namna gani ya kufanikisha uwepo wa kituo cha kuuzia na kununulia madini Wilayani Liwale kwani Jiografia ya Wilaya hiyo inafanya utoroshaji wa madini kuwepo kutokana na soko la madini kuwepo sehemu moja ambayo ni Ruangwa.

Awali akimkaribisha mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mtendaji Mkuu wa GST, DKT. Mussa Budeba amewasihi wachimbaji wa Madini wa Mkoa wa Lindi kuendelea kutumia taarifa za kitaalam katika utafutaji na uchimbaji madini na kuahidi kuwa GST itaendelea kushirikiana nao kwa kuwapatia elimu, taarifa za kitaalam, utafiti na uchunguzi wa sampuli zao.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!