

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tamisemi na Mbunge wa Rufiji, Mhe. Muhamed Mchengerwa, amemtaka mkandarasi wa kampuni ya Nyanza Road Works kuongeza kasi katika ujenzi wa daraja la Mbambe ili likamilike kwa wakati na kuondoa changamoto zinazowakabili wananchi.
Akizungumza leo, Machi 18, 2025, katika ziara yake ya kukagua ujenzi wa daraja hilo katika kijiji cha Mbamwe, wilaya ya Rufiji, Mchengerwa alisema kuwa kiwango cha asilimia 22 kilichofikiwa hadi sasa ni kidogo sana.
“MKandarasi, ongeza kasi ya ujenzi wa daraja hili kwani asilimia 22 iliyofikiwa bado ni ndogo sana. Katika mwendo huu, mvua zikiongezeka zitaleta changamoto itakayokwamishe ujenzi,” alisisitiza Mchengerwa.

Aidha, Mchengerwa aliwataka wananchi wa eneo hilo kushirikiana na viongozi wa Wilaya kwa kutoa taarifa pale wanapoona hali ya kudorora katika ujenzi wa daraja hilo. Aliwatoa hofu wananchi kuhusu fidia kwa kusema kuwa Rais Samia Suluhu Hassan tayari ametoa fedha kwa ajili ya fidia kwa wale wote ambao mali zao zimeathirika na mradi huo, ambao pia unahusisha ujenzi wa barabara za maingiliano zenye urefu wa kilomita 3.
Kwa upande wake Mhandisi Emmanurel Owaya kutoka kampuni ya Nyanza Road Works amesema kuwa ujenzi umefikia asilimia 22, huku nguzo za msingi 64 kati ya 107 zikiwa zimejengwa. Aliongeza kuwa shilingi bilioni 24.16 zinatarajiwa kutumika kukamilisha ujenzi wa daraja hilo, ikiwa ni pamoja na barabara za maingiliano za kilomita 3 kwa pande zote mbili za daraja.