Home Kitaifa WAMILIKI WA KAMPUNI NA TAASISI BINAFSI WATAKIWA KUHAMASISHA NA KUZIPATIA OZOEFU KAMPUNI...

WAMILIKI WA KAMPUNI NA TAASISI BINAFSI WATAKIWA KUHAMASISHA NA KUZIPATIA OZOEFU KAMPUNI ZINAZOCHIPUKIA

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa wamiliki wa kampuni na taasisi binafsi nchini kuhamasisha na kuzipatia uzoefu kampuni zinazochipukia (business startups) ambazo zitakuwa chachu ya mageuzi makubwa ya baadae ili kuongeza wigo wa Sekta Binafsi hapa nchini.

Makamu wa Rais pia amesema  Serikali imedhamiria kufanya kazi na Sekta Binafsi katika miradi mbalimbali ya ubia kama vile ujenzi wa barabara, miradi ya umwagiliaji na uzalishaji wa nishati hivyo ameiagiza Wizara ya Fedha na Mipango kwa kushirikiana na TPSF kukaa pamoja na kuangalia namna ya kuongeza ushiriki wa Sekta hiyo katika miradi ya ubia ili kukabiliana na mwitikio mdogo uliopo.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati wa maadhimisho ya siku ya sekta binafsi 2022 nchini Tanzania iliofanyika Disemba 2, 2022 Jijini Dar es salaam.

Pia Makamu wa Rais amewasisitiza wadau wote wa Sekta Binafsi chini ya TPSF kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais  – Mazingira, Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, na Ofisi za Ubalozi kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuchangamkia rasilimali fedha za kulinda mazingira kama vile biashara ya hewa ukaa na Green Climate Fund  kuibua miradi ya utunzaji wa mazingira ikiwa pamoja na utengenezaji wa nishati mbadala, viwanda vya kuchakata taka ngumu na miradi mingine ya aina hiyo. 

Aidha amesema Serikali imeendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji hapa nchini kwa lengo kuu la kuvutia uwekezaji, kukuza biashara na kukuza ushindani wa Sekta Binafsi.
Hivyo ameiagiza Wizara ya Viwanda na Biashara kuongeza kasi ya utekelezaji wa Mpango wa Maboresho ya Mazingira ya Biashara (National Blueprint) kwa kuhakikisha wanatekeleza shughuli zilizopangwa katika Mpango huo kufikia asilimia 50 mwezi Disemba 2023 kutoka kiwango cha sasa cha asilimia 13 na kuzichukulia hatua taasisi ambazo hazitaki kubadilika na zinakwamisha utekelezaji wa Blueprint.  

Kwa upande wake Waziri wa Viwanda na Uwekezaji Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) amesema Serikali kupitia wizara hiyo imeendelea na jitihada za kuweka mazingira wezeshi ili kuweza kutumia vema eneo huru la biashara Barani Afrika kwa manufaa ya taifa ikiwemo sekta binafsi. Ametoa wito kwa sekta binafsi kuweza kulifikia soko hilo kwa kupeleka bidhaa zinazoweza kununulika na zenye uzalishaji endelevu.

Awali akitoa taarifa ya maendeleo ya Sekta Binafsi nchini , Mwenyekiti wa Sekta hiyo Bi. Angelina Ngalula ameishukuru serikali kwa mazingira bora na yenye haki ya ufayaji biashara nchini pamoja kudhibiti kwa kiasi kikubwa mfumuko wa bei,kuimarisha mahusiano ya sekta binafsi na ya Umma nchini, kuondolewa kwa vikwazo vya kibiashara katika masoko ya kikanda pamoja na kufunguliwa kwa masoko makubwa ya kimataifa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!