Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa wito kwa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (DAWASA) kuendelea kutafuta vyanzo vipya vya maji na kuviingiza kwenye mfumo.
Amesema kuwa licha ya kuongezeka kwa kiwango cha maji kwenye mfumo wa uzalishaji na usambazaji, wasilale bali waendelee kuwatumia wataalam wa ndani kutafuta maji zaidi.
Amesema hayo leo (Novemba 29, 2022) alipotembelea eneo la mradi wa maji Kisarawe mjini, mkoani Pwani.
Amesema kuwa kumekuwa na ongezeko la makazi, viwanda na shughuli mbalimbali za kujamii ambazo kwa kiasi kikubwa zinahitaji uwepo wa maji ya kutosha. “Tusilale tuendelee na uzalishaji wa maji, Tunataka huduma hii isambae na iwafikie watu wote”
“Ndugu wafanyakazi wa DAWASA mnapaswa kutambua maji ni huduma nyeti kwenye maisha ya binadamu, kazi yenu inahitaji uaminifu na uadilifu mkubwa, fanyeni kazi hii ya umma, wahudumieni watanzania, tambueni maeneo yenye uhitaji na mpeleke huduma”