Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amezitaka Halmashauri zote nchini kuongeza nguvu ya kusimamia miradi mingine ya maendeleo baada ya kutekeleza kwa mafanikio miradi ya mpango wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19.
Amesema kuwa Halmashauri zimekuwa zikisimamia utekelezaji wa miradi itokanayo na fedha za Mpango wa UVIKO-19 tu ikiwa zilishapokea fedha za miradi mingine ikiwemo EP4R na mradi wa kuimarisha ubora wa Elimu ya Sekondari (SEQUIP).
Amesema hayo kwa nyakati tofauti leo (Jumapili, Novemba 27, 2022) alipokagua miradi ya maendeleo na kuzungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga akiwa katika ziara ya kikazi ya siku tatu mkoani Pwani.
“Fedha zimekuja lakini kila ninapokwenda ninapewa taarifa ya miradi ya UVIKO-19 tu, sasa nitataka taarifa ya fedha ya miradi mingine imefanya nini na majengo yake yamefikia hatua gani, wengi mmejificha kwenye koti la miradi ya UVIKO”
Akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga Mheshimiwa Majaliwa amewataka watumishi wa umma kufanya kazi kwa weledi, uamimifu na kujitoa katika kuwahudumia watanzania “Serikali imejipanga vizuri kuwahudumia watanzania”
Kadhalika Waziri Mkuu ameagiza TAKUKURU mkoa wa Pwani kufanya uchunguzi dhidi ya Mfamasia wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga Edwin Clemence Feruzi kwa kushindwa kutekeleza majukumu yake kwa weledi na kukiuka miiko ya kazi.
Aidha Mheshimiwa Majaliwa amemtaka Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga Bi. Khadija Nasr Ali kuhakikisha mpaka kufikia Disemba 30 mwaka huu watumishi wanaofanya kazi kwenye Halmashauri hiyo lakini wanaoishi Dar es Salaam wawe wamerejea na kuishi katika eneo la kazi.