Home Kitaifa DKT.BITEKO AUAGIZA MGODI WA ALMASI MWADUI KUKAMILISHA TATHMINI YA AJALI

DKT.BITEKO AUAGIZA MGODI WA ALMASI MWADUI KUKAMILISHA TATHMINI YA AJALI

Mkuu wa Mkoa aunda Kamati kuchunguza chanzo, athari na kutoa mapendekezo

Serikali kuchukua hatua kudhibiti madhara kutokea

Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko ameuagiza Mgodi wa Almasi wa Williamson Diamond Limited (WDL) kukamilisha tathmini ya ajali ya kubomoka kwa bwawa la tope na kuathiri sehemu ya makazi ya watu yanayozunguka eneo la mgodi.

Dkt. Biteko ametoa agizo hilo Novemba 10, 2022 akiwa katika eneo la Mgodi wa WDL wilayani Kishapu Mkoa wa Shinyanga kwa lengo la kubaini athari zilizojitokeza baada ya bwawa la mgodi huo kubomoka Novemba 7, 2022 na kuleta athari kwa mgodi na jamii zinazozunguka mgodi.

Ameutaka mgodi huo kukamilisha kufanya tathmini ya wote waliopata madhara katika mashamba yao, mifugo na makazi ili walipwe fidia na mgodi huo.

Aidha, Dkt. Biteko ameutaka mgodi wa WDL kuharakisha kufanya tathmini ili shughuli za uzalishaji katika mgodi ziweze kuendelea katika muda uliopangwa.

Pia, amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga kwa kuunda Kamati maalum inayochunguza chanzo cha bwawa kubomoka, kutambua athari zilizojitokeza na kutoa mapendekezo kwa Serikali kuhusu tukio hilo.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Sophia Mjema, ameahidi kutekeleza maagizo yote yaliyotolewa na Waziri wa Madini ikiwemo kusimamia Kamati iliyoundwa kufanya tathmini ili iweze kukamilisha kwa haraka.

Naye, Mbunge wa Jimbo la Kishapu Boniphace Butondo ameiomba Kamati iliyoundwa kuhakikisha inatenda haki katika mchakato mzima wa tathmini ili wananchi walioathirika wapate haki zao.

Kwa upande wake Meneja Mkuu wa Mgodi wa WDL, Mhandisi Ayoub Mwenda, amesema hadi sasa watu 115 waliojitokeza kutokana na kuathiriwa na tukio wamehifadhiwa katika mazingira salama na kupatiwa huduma zote stahiki ikiwa ni pamoja na wanafunzi kupelekwa shuleni.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!