Home Kitaifa NAIBU WAZIRI MAVUNDE AZINDUA UJENZI WA MIUNDOMBINU YA UMWAGILIAJI KWENYE MASHAMBA YA...

NAIBU WAZIRI MAVUNDE AZINDUA UJENZI WA MIUNDOMBINU YA UMWAGILIAJI KWENYE MASHAMBA YA MBEGU YA ASA

Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Anthony Mavunde amezindua rasmi ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji katika mashamba ya uzalishaji mbegu yaliyo chini ya Wakala wa Mbegu za Kilimo(ASA) ikiwa ni utekelezaji wa mpango wa Serikali wa kuzalisha mbegu bora kipindi cha kiangazi ili kuondoa changamoto ya uhaba wa mbegu na kuongeza upatikanaji wake unapofika msimu wa kilimo,mradi ambao utagharimu kiasi cha Tsh Bilioni 18.

Uzinduzi huo umefanyika leo tarehe 04 Novemba, 2022 katika shamba la mbegu la Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) la Msimba lililopo Kilosa mkoani Morogoro.

Dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan ni kuondoa changamoto zinazomkabili mkulima, mojawapo ikiwa ni ya upatikanaji hafifu wa mbegu bora msimu wa kilimo. Ndiyo maana, Mhe. Rais ametuongezea fedha za bajeti ili tuweze kuweka miundombinu ya umwagiliaji kwenye mashamba ya mbegu ambayo itapelekea mbegu bora kuzalishwa kabla ya kuanza kwa msimu wa kilimo”

Visima vitano virefu vya maji vilivyochimbwa hapa vitasaidia kuzalisha maji yatakayohifadhiwa katika bwawa lenye uwezo wa kuhifadhi maji lita milioni 45.

Huu ni mwanzo wa mabadiliko makubwa yanayokuja katika uzalishaji wa mbegu bora hapa nchini ili tufikie lengo la uzalishaji wa mbegu wa kutosheleza mahitaji ya nchi na kupata ziada ya kuuza nje ya nchi.

ASA hakikisheni mnaishirikisha sekta binafsi katika uzalishaji wa mbegu bora kwakuwa ili tuweze kufikia malengo lazima tuunganishe nguvu kwa pamoja baina ya serikali na sekta binafsi na kamwe hampaswi kuwa washindani bali mtegemeane kwa manufaa ya nchi.

Nakuagiza Mtendaji Mkuu wa ASA, Dkt. Sophia Killenga-Kashenge kuhakikisha mashamba yote ya ASA yanalimwa na kuongeza uzalishaji wa mbegu, badala ya kuyaacha kama mapori kama ilivyo sasa sambamba na kuwekewa uzio ili kuyalinda na uvamizi kutoka kwa watu mbalimbali ambao wanayaona kama hayatumiki.

Hivyo niwaombe wadau wote tushirikiane kwa pamoja katika kutekeleza mipango ya serikali kukuza sekta ya kilimo kupitia utekelezaji wa Vipaumbele vya Wizara ya Kilimo kupitia Ajenda 10/30 ambavyo ni kuimarisha utafiti, kuongeza uzalishaji wa mbegu, kuimarisha huduma za ugani, umwagiliaji na kuwezesha upatikanaji wa masoko ya uhakika kwa mazao ya wakulima”Alisema Mavunde

Naye mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Alhaj Majid Mwanga aliishukuru Serikali kwa kupeleka mradi huo mkubwa Kilosa na kusisitiza kuwa wataendelea kushirikiana na ASA bega kwa bega ili mradi huo uweze kuleta tija kwa wananchi wa Kilosa na Tanzania kwa ujumla.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!