Home Kitaifa RAIS SAMIA AWAPAISHA WANAWAKE KATIKA SEKTA YA MADINI

RAIS SAMIA AWAPAISHA WANAWAKE KATIKA SEKTA YA MADINI

📌 Dkt. Biteko asema uwezo wa wanawake sekta ya madini hautiliwi shaka

📌 Ushiriki wa wanawake katika madini kukuza mnyororo wa thamani

📌 Sh. Bilioni 10 kuwezesha wanawake wachimba madini ngazi ya chini

Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kufungua fursa mbalimbali za kuwawezesha wananchi kiuchumi ikiwa ni pamoja na kuzitilia mkazo ushirikishaji wa wanawake katika uchimbaji wa madini wenye tija.

Dkt. Biteko amesema hayo Februari 28, 2025 jijini Dar es salaam wakati aliposhiriki kongamano maalum kuelekea Maadhimisho Siku ya Kimataifa ya Wanawake (Pre IWD) ambapo amesema kwa sasa kuna ongezeko kubwa la wanawake wanaoshiriki katika Sekta ya madini ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikitawaliwa na wanaume na kwa mujibu wa Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022, watu 6,030,575 wanajihusisha na shughuli mbalimbali katika mnyororo wa thamani katika sekta ya madini.

Kufuatia takwimu hizo, wanawake ni 3,094,647 sawa na asilimia 51.3 ya watu wote wanaojihusisha na shughuli mbalimbali katika uchimbaji mdogo wa madini hususan katika sekta ndogo ya u ziduaji. Aidha, kati ya wachimbaji wadogo milioni moja na nusu, asilimia 27 kati yao ni wachimbaji ni wanawake.

Ametaja jitihada za Rais Samia katika kukuza ushiriki wa wanawake katika sekta hiyo kuwa ni kutoa kipaumbele wanawake kushiriki katika shughuli zote za Kiuchumi kwa kuwapa fursa za elimu pamoja na kumiliki rasilimali zilizopo kama vile kupata elimu, fursa za kupata mikopo yenye masharti nafuu pamoja na kupata vifaa na vitendea kazi na kushiriki katika vikao mbalimbali vya maamuzi.

Amefafanua kuwa ushiriki wa wanawake katika sekta ya madini ni nyenzo muhimu katika kukuza mnyororo wa thamani katika jamii na hivyo ni muhimu kutambua na kuthamini mchango wao katika shughuli hizo na jamii kwa ujumla.
Aidha, taarifa kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Sekta ya Madini ikijumuisha na masuala ya gesi, kwa mwaka wa fedha wa 2020/2021 imechangia kwa kiasi kikubwa katika ajira. Ambapo ajira za moja kwa moja 218,353. Kati ya ajira hizo, 176,815 ni wanaume na 41,538 ni wanawake ambayo ni sawa na asilimia 20.

Amesema Serikali imetekeleza na kuweka mazingira wezeshi kwa wanawake kushiriki kikamilifu katika sekta hiyo kupitia utekelezaji wa Sera wezeshi, Sheria na taratibu mbalimbali ambapo kupita Sera ya Taifa ya Jinsia na Maendeleo ya Wanawake ya mwaka (2023) na Sheria ya Madini ya mwaka (2017) pamoja na kanuni za ‘Local Content’, Serikali inasisitiza ushirikishaji wa wanawake na kuhakikisha wanapata uwezo rasilimali katika sekta ya madini.

Vilevile, uwezeshaji wa kifedha na kitaaluma, ambapo Serikali kupitia Taasisi zake na wadau mbalimbali ikiwemo Kamisheni ya Madini Tanzania na Umoja wa Wachimba Madini Wanawake Tanzania (TAWOMA), imesadia kutoa mafunzo ya kitaalam kwa wanawake mbalimbali ndani na nje ya nchiambapo mwaka 2023, Serikali iliwapeleka wanawake watano nchini China kwa ajili ya kujifunza na kutafuta masoko.

“Jumla ya kiasi kisichopungua shilingi bilioni 10 kimeelekezwa katika kuwezesha miradi na shughuli mbalimbali za wanawake wachimba madini kwa ngazi ya chini. Aidha, katika mitambo ya uchorongaji 10 iliyonunulwa na Serikali kupitia STAMICO mitambo miwili itakabidhiwa kwa wachimbaji wanawake kupitia TAWOMA,”amesisitiza Dkt. Biteko.

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amesema ushirikiano wa sekta ya umma, Sekta binafsi na wadau wengine ni muhimu katika kuinua ushiriki wa wanawake katika sekta hiyo muhimu ya uziduaji.

Naye Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde amewapongeza waandaaji wa kutaniko hilo chini ya Christer Mhingo kuendeleza ushiriki wa wanawake katika sekta hiyo ya uziduaji.

“Bi Christer amekuwa balozi mzuri wa sekta ya uziduaji ndani na nje ya nchi, amekuwa akizitangaza fursa za utalii zilizopo nchini. Wizara tutaendelea kumuunga mkono ili atimize malengo yake,” amesema Waziri Mavunde.

Halikadhalika, amemshukuru Rais Samia kwa kuweka jitihada mbalimbali ikiwemo mabadiliko ya Sheria ya mwaka 2017 ambayo yamesaidia kuongeza ushiriki wa wanawake katika sekta ya madini kuanzia uchimbaji hadi kuongeza thamani.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Mwanaidi Ali Khamis amesema maono ya Rais Samia ys kuunda inayoshughulikia masuala ya wanawake moja kwa moja ni moja ya chachu katika ukombozi wa wanawake wakiwemo wale wanaofanya kazi katika sekta ya madini.

“Mheshimiwa Rais alivyoona kuna umuhimu wa kuwawezesha wanawake kwa karibu zaidi ndipo akaunda upya Wizara ambayo ndani yake kuna kipengele kinachoshughulikia masuala ya wanawake. Ndiyo maana tunasema Samia…” amesema Naibu Waziri Mwanaidi.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Azurite Management and Consultancy na waandaji wa tukio la awali kuelekea Maadhimisho ya Siuku ya Wananwake (Pre International Women’s Day), Bi. Christer Mhingo amesema kuwa Taasisi yake iliandaa programu mbalimbali katika maeneo tofauti tofauti na wamekutana na wanafunzi wa shule ya msingi na sekondari kwa ajili ya kusaidia wanawake waliopo kwenye sekta ya uchimbaji madini.

MWISHO

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!