
Maafisa maendeleo ya jamii pamoja na watendaji wa serikali wilayani Nyang’hwale, mkoani Geita, wametakiwa kuendelea kutoa elimu kwa vijana kuhusu matumizi sahihi ya mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na serikali, ili kuwawezesha kujikwamua kiuchumi na kuachana na utegemezi.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Geita, wakati wa ziara yake ya kukagua uhai wa chama katika kata 122 za mkoa huo.
Amesema ni jukumu la maafisa maendeleo kuwawezesha vijana kuunda vikundi na kuhakikisha wanapata mikopo kwa wakati, ili waweze kuinuka kiuchumi na kuongeza kipato. Ameeleza kuwa hatua hiyo itasaidia kupunguza tatizo la matumizi ya dawa za kulevya na vijana kukaa mitaani bila ajira.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Nyang’hwale, Hussein Kassu, ameeleza kuwa kiasi cha shilingi milioni 800 kimeshindwa kutolewa kama mikopo kwa vikundi vya vijana kutokana na ukosefu wa mfumo rafiki wa kuwawezesha kukopa.
Baadhi ya vijana wamekiri kutokuwa na uelewa wa kutosha kuhusu utaratibu wa kuomba mikopo na jinsi ya kuunda vikundi vyao, huku wakieleza kuwa walikuwa wakisubiri kutembelewa na maafisa maendeleo kwa ajili ya ukaguzi.
Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Geita tayari ametembelea kata 10 katika Wilaya ya Nyang’hwale, ambako amekutana na wanachama wa chama hicho na kueleza miradi ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.