Home Kitaifa RAIS SAMIA: DHAMIRA YA SERIKALI NI KUINUA SEKTA YA KILIMO KWA KUONGEZA...

RAIS SAMIA: DHAMIRA YA SERIKALI NI KUINUA SEKTA YA KILIMO KWA KUONGEZA TIJA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa serikali imejipanga kuhakikisha wakulima wanalima kwa tija mwaka mzima kwa kuwekeza katika miradi mikubwa ya umwagiliaji, ikiwemo Bwawa la Mkomazi ambalo litakuwa na uwezo wa kuhifadhi zaidi ya lita bilioni 70 za maji kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Chuo cha Ualimu Korogwe leo Jumatatu Februari 24, 2025, Rais Samia amesema kuwa, mradi huo utawanufaisha wakulima zaidi ya 20,000 na utasaidia kuondoa utegemezi wa mvua katika kilimo.

Nimempa Waziri wa Kilimo Shilingi bilioni 18.2 kwa ajili ya kuwezesha wakulima kushiriki shughuli za kilimo, waweze kulima mara mbili hadi mara tatu kwa mwaka. Kwa uwepo wa mradi huu, wakulima sasa watalima bila kutegemea mvua na kupata mavuno zaidi” alisema Rais Samia.

Ameongeza kwa kusema kuwa, dhamira ya serikali ni kuinua sekta ya kilimo kwa kuongeza tija na kuhakikisha Tanzania inakuwa na chakula cha kutosha huku pia ikiuza mazao nje ya nchi.

Aidha, Rais Samia amewataka viongozi wa Mkoa wa Tanga kuendelea kusimamia vizuri fedha zinazotolewa kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo, akisisitiza kuwa miradi mingi inatekelezwa kwa ufanisi mkubwa.

Katika hotuba yake, Rais Samia pia amewakumbusha wananchi kuhusu umuhimu wa kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura ili kuhakikisha wanapata haki ya kushiriki uchaguzi wa mwezi Oktoba mwaka huu.

Kama jina lako halipo kwenye daftari la wapiga kura, hutaweza kupata haki yako ya kupiga kura. Kama unafurahia maendeleo na miradi inayoletwa Korogwe, hakikisha umejiandikisha ili upate sifa na haki ya kupiga kura,” alisisitiza Rais Samia.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!