
Na Shomari Binda
MBUNGE wa jimbo la Musoma mjini Vedastus Mathayo ameendelea kuwasemea wananchi bungeni kuhusiana na masuala mbalimbali.
Leo februari 14 bungeni katika bunge la 12 mkutano wa 18 mbunge huyo katika swali la nyongeza alilouliza kwenye Wizara ya Ulinzi alitaka kujua ni nini kinaendelea katika eneo la jeshi Makoko kuhusu ujenzi wa shule.
Mbunge Mathayo amesema katika siku za nyuma alishaulizia kuhusu eneo hilo na timu ya Wizara kufika eneo la tukio lakini bado majibu hayajapatikana.
Amesema wananchi wa eneo la Makoko manispaa ya Musoma wanao uhitaji mkubwa wa shule ili watoto wa eneo hilo waweze kupata elimu.
” Mheshimiwa Naibu Spika nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza,katika siku za nyuma niliuliza hapa bungeni kuhusu eneo la jeshi Makoko pale Musoma kuhusu maombi ya wananchi na ujenzi wa shule.
” Nashukuru timu ilishafika pale na kuangalia eneo hilo sasa nini kinaendelea ili wananchi waelewe kuhusu maombi yao”ameulizia.
Akimjibu mbunge huyo kwa swali aliloulizia Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Innocent Bashungwa amesema hatua ya kufika eneo la tukio na kuangalia ni hatua kubwa iliyofikiwa.
Bashungwa amempongeza mbunge Vedastus Mathayo kwa ufatiliaji wake katika kuwasemea wananchi wa jimbo la Musoma mjini na kudai jambo likikamilika watapata majibu kuhusu eneo hilo la Makoko.