Na Shomari Binda-Musoma
MJUMBE wa Kamati ya Utekelezaji ya Jumuiya ya Wazazi wa CCM Taifa Mgore Miraji amewaasa vijana wa Jumuiya ya Vijana wa CCM( UVCCM) Musoma mjini kuzingatia maadili na kuheshimu wazazi.
Kauli hiyo imetolewa leo februari 12/2025 kwenye kikao cha baraza la vijana wa CCM Musoma mjini lililofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa CCM mkoa wa Mara.
Amesema mmomonyoko wa maadili kwenye jamii umekuwa mkubwa hivyo vijana wa CCM wanapaswa kuwa mfano wa kuigwa kwa maadili mazuri.
Mgore ambaye alikuwa mgeni mualikwa kutoka jumuiya ya wazazi na Kamati ya Siasa ya Wilaya amesema yeye kama mzazi ujumbe mkubwa kwa vijana ni suala la maadili.
Amesema kijana anapokuwa na maadili mazuri anaaminiwa kwenye chama na jamii inayomzunguka hivyo kupata fursa mbalimbali zikiwemo nafasi za uongozi.
Aidha Mgore amemsaidia mmoja wa vijana wa CCM meno mawili ya bandia baada ya kudondoka wakati wa kampeni za uchaguzi wa serikali za mitaa.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Musoma mjini Magiri Benedict amesema vijana ni nguzo ndani ya chama ambao wanapaswa kukilinda kwa nguvu zote.
Amesema muda wa uchaguzi ukifika wao pia wanayo nafasi ya kujitokeza na kuomba nafasi za uongozi zikiwemo za udiwani na ubunge kwa kuwa sasa vijana ni taifa la leo na sio kesho.
Kwa upande wake Mjumbe wa Kamati ya Elimu Malezi na Mazingira na diwani wa viti maalum manispaa ya Musoma Asha Muhamed amesema maadili kwa vijana ni pamoja na kuheshimu viongozi na jamii nzima.
Akifunga kikao cha baraza la vijana wa CCM ( UVCCM)Wilaya ya Musoma, Mwenyekiti wa jumuiya hiyo Kassim Juma amewataka vijana kuzingatia yaliyozungumzwa na viongozi wa chama
Amesema suala la maadili limesisitizwa na viongozi hivyo vijana wanapaswa kuzingatia na kuishi ndani ya maadili mazuri.