Home Kitaifa KATIBU TAWALA WA MKOA WA GEITA AZINDUA BODI MPYA YA USHAURI YA...

KATIBU TAWALA WA MKOA WA GEITA AZINDUA BODI MPYA YA USHAURI YA HOSPITALI YA RUFAA

Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita, Mohamed Jumanne Gombati, amezindua rasmi Bodi mpya ya Ushauri ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita na kuitaka bodi hiyo pamoja na uongozi wa hospitali kufanya kazi kwa mshikamano ili kufanikisha malengo ya serikali ya kuboresha huduma za afya.

Akizungumza wakati wa kikao cha kwanza cha bodi hiyo, Gombati alisisitiza umuhimu wa bodi hiyo katika usimamizi wa huduma za afya na kuhakikisha utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

“Bodi ya ushauri ya Hospitali ya Rufani ya Mkoa, ni chombo muhimu sana katika uendeshaji wa huduma za afya za Hospitali. Ni kiungo kinachowaunganisha wananchi na serikali yao na kuboresha utoaji wa huduma,” amesema Gombati

“Kazi kubwa ya bodi ni kuisimamia karibu sana menejimenti ya hospitali katika utekelezaji wa majukumu yake, kimsingi menejmenti ya hospitali inawajibika moja kwa moja kwa bodi, hivyo wajumbe tumieni taaluma zenu kuisaidia hospitali katika uendeshaji wa huduma za afya,” ameongeza.

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita, Dkt. Omary Sukari, alisema bodi hiyo itasaidia kuhakikisha wananchi wanapata wawakilishi wa kutoa maoni yao kuhusu huduma za afya zinazotolewa hospitalini hapo.

Aidha, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita, Dkt. Mfaume Kibwana, alieleza kuwa hospitali hiyo inaendelea kuboresha huduma mbalimbali za kibingwa, ikiwemo huduma ya CT Scan, ambayo imepunguza rufaa za wagonjwa kwenda hospitali za mbali.

Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya hospitali hiyo, Manase Ndoroma, ameishukuru serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kuwaamini na kuwateua kusimamia hospitali hiyo. Ameahidi kuwa bodi itatekeleza majukumu yake kwa ufanisi ili kuboresha huduma za afya kwa wakazi wa Geita.

Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita ilianza kama hospitali ya halmashauri mnamo Juni 2016 baada ya Wizara ya Afya kuiteua rasmi ili kutoa huduma za rufaa kwa mkoa pamoja na kusaidia vituo vya afya vya ngazi za chini na taasisi za mafunzo.

Kwa mujibu wa Sensa ya Taifa ya mwaka 2022, Mkoa wa Geita una wakazi 2,977,608, ambapo wanaume ni 1,463,764 na wanawake ni 1,513,844. Hospitali hii inahudumia Halmashauri za Mji wa Geita, Geita, Chato, Bukombe, Mbogwe, na Nyang’hwale.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!