![](https://www.mzawa.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/IMG-20250209-WA0155-1024x641.webp)
Na Shomari Binda-Serengeti
MBUNGE wa viti maalum mkoa wa Mara Ghati Chomete amemuhakikishia Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi ( CCM) Bara Stephine Wasira kura za kishindo za Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwenye uchaguzi mkuu wa 2025.
Ghati amemuhakikishia kiongozi huyo kura hizo ikiwa ni siku ya mwisho ya ziara yake mkoani Mara mara baada ya kuchaguliwa kwenye nafasi hiyo.
Amesema kwa namna ambavyo kazi kubwa imefanywa na Rais Samia ikiwa ni pamoja na kutoa fedha nyingi za miradi ya maendeleo kura zitakuwa za kutosha.
Mbunge huyo amesema mkoa wa Mara katika sekta ya elimu umenufaika ikiwa ni pamoja na kujengwa shule mpya zilizowezesha watoto wa mkoa wa Mara kupata elimu.
Amesema licha ya sekta ya elimu upande wa maji,afya na miundombinu miradi mbalimbali imeendelea kutekelezwa mkoa mzima wa Mara.
Mbunge huyo amesema mwanamke wa mkoa wa Mara kupitia miradi ya maji na kutuliwa ndoo kichwani watatoa shukrani kwa kumpigia kura za kishindo Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan.
” Mheshimiwa Makamu Mwenyekiti tufikishie salamu zetu kwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan na tunamuhakikishia kura za kishindo kutoka mkoa wa Mara kwenye uchaguzi wa mwaka 2025.
” Mama Samia katufanyia mambo makubwa mkoa wa Mara na hatuna deni nae bali yeye ndiye anatudai na tutamlipa kwa kumpigia kura za kishindo”,amesema.
Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara Stephine Wasira amekamilisha ziara yake mkoani Mara kwa kuzitembelea Wilaya 6 za mkoa huo.
![](https://www.mzawa.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/IMG-20250209-WA0156-1024x768.webp)