![](https://www.mzawa.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/IMG-20250206-WA0004-1.webp)
![](https://www.mzawa.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/IMG-20250206-WA0006.webp)
Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT) kimeendesha mafunzo jumuishi kwa vitendo kwa wanafunzi wa Astashahada na Stashada, ambapo wanafunzi wameonesha kwa vitendo kile walichojifunza katika muhula wa kwanza wa masomo.
Akizungumza katika hafla fupi wakati wa mafunzo hayo, Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Taaluma, Tafiti na Ushauri, Bi. Jesca William, amesema mafunzo kwa vitendo ni muhimu kwani yanawaimarisha wanafunzi na kuwawezesha kupata ujuzi utakaowasaidia kumudu soko la ajira mara baada ya kumaliza masomo yao.
![](https://www.mzawa.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/IMG-20250206-WA0005-1.webp)
“Kwa tukio hili, wanafunzi wanatuhakikishia kuwa wako tayari kuingia kwenye soko la ajira. Sisi ni chuo kinachojikita kwenye vitendo ili mwanafunzi akimaliza masomo aweze kushindana kwenye soko la ajira, ndani na nje ya nchi, sambamba na kujiajiri mwenyewe,” amesema Bi. Jesca.
Aidha, amewapongeza walimu kwa kujitoa katika kuhakikisha kuwa wanafunzi wanapata mafunzo stahiki kwa nadharia na vitendo, huku akiwataka wanafunzi kuendelea kushirikiana na kusoma kwa bidii ili kufanikisha malengo yao.
![](https://www.mzawa.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/IMG-20250206-WA0007.webp)
Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Taaluma wa chuo hicho, Bi. Claudia Nshekanabo, amesema mafunzo hayo yanawapima wanafunzi kwa vitendo katika utoaji wa huduma kulingana na walichojifunza darasani.
Ameeleza kuwa mafunzo hayo yamehusisha Idara ya Uratibu wa Matukio na Ukarimu, ambapo wanafunzi wamejifunza kutoa huduma kwa wageni na watalii, zikiwemo huduma za vyakula, vinywaji, malazi, na uratibu wa matukio.
“Mafunzo haya yamehusisha wanafunzi 30 wa Astashahada na Stashada kutoka muhula wa kwanza wa masomo. Hufanyika kila muhula mpya unapokaribia kumalizika, kabla ya kuingia kwenye mitihani,” amesema Bi. Nshekanabo.
Naye, Dorothea Gangai, mwanafunzi wa mwaka wa pili katika fani ya Sanaa ya Upishi, amewashukuru walimu wa chuo hicho kwa kuwajengea uwezo, akisema kuwa wamekuwa mahiri katika fani zao hata kabla ya kuhitimu masomo.
“Tunawashukuru sana walimu wetu. Wanatufundisha mpaka tunaelewa. Hata kama mtu atakuja na uelewa mdogo, ataondoka na ujuzi wa kutosha. Walimu wanatoa ushirikiano wa hali ya juu sana,” amesema Gangai.
Chuo cha NCT huendesha mafunzo haya kila muhula wa masomo unapomalizika kwa lengo la kuwapima wanafunzi wao kuelekea katika ratiba ya mitihani.