![](https://www.mzawa.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/IMG-20250205-WA0081-1024x682.webp)
📌 Lengo ni wananchi kuepuka gharama inayotokana na kuunganisha umeme wakati miradi imekamilika
Naibu Waziri wa Nishati, Mhe Judith Kapinga ametoa rai kwa wananchi kuunganisha huduma ya umeme wakati miradi mbalimbali ya umeme inapotekelezwa ili kuepuka gharama inayoweza kutokea pale miradi inapokuwa imekamilika.
Mhe. Kapinga ameyasema hayo leo Februari 05 2025 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la la Mbunge wa Tanga Mjini Mhe. Ummy Mwalimu aliyetaka kufahamu Serikali ina mkakati gani wa kuwaunganishia umeme wa gharama nafuu kwa Wananchi wa maeneo ya Pembezoni yenye sifa za Vijiji mkoani Tanga.
“Katika kurahisisha upatikanaji wa huduma ya umeme wa bei nafuu kwa maeneo ya pembezoni mwa Jimbo la Tanga Mjini, Serikali kupitia REA inaendelea kutekeleza Mradi wa Peri-Urban III”, Amesema Mhe. Kapinga.
![](https://www.mzawa.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/IMG-20250205-WA0085-1024x682.webp)
Ameongeza kuwa mradi huo unatekelezwa na Mkandarasi OK Electrical kwa kuunganisha wateja kwa baadhi ya mitaa kwa gharama ya shilingi 27,000 ambapo mpaka sasa jumla ya wateja 1,302 wameshaunganishiwa huduma ya umeme. Mhe. Kapinga amesema maeneo ya Tanga Mjini yaliyosalia yapo kwenye mradi wa kupeleka umeme kwenye vitongoji 15 vya kila Mbunge (HEP IIA) ambapo Jimbo la Tanga Mjini litapelekewa umeme kwenye mitaa 15.
Akielezea kuhusu Serikali kuanzisha utaratibu wa kuwaunganishia umeme wananchi kwa mkopo, Mhe. Kapinga amesema Serikali inatekeleza miradi mbalimbali ya umeme ili kuwafikia wananchi kwa gharama nafuu ya shilingi 27,000/-.
Mhe. Kapinga ameongeza kuwa TANESCO ilishawahi kuwaunganishia wananchi kwa kuwakopesha ambapo ilikutana na changamoto ya wananchi kutokuwa na utayari ya kulipa madeni yao.
Akijibu swali Mbunge wa Ilemela, Mhe. Angelina Mabula aliyetaka kufahamu mitaa ya Masenene, Kilabela, Bujingwa, Nyanguku, Butimba na Toronto itapatiwa umeme kutokana na kuondolewa katika mitaa 15 inayotekelezwa na REA kutokana na kuwepo kwa njia kubwa ya umeme.
Akijibu swali hilo Mhe. Kapinga amesema miradi ya vitongoji ni ya ujazilizi ambayo inajumuisha ujenzi wa miundombinu ya umeme kwenye maeneo ambayo yamepitiwa na njia kubwa ya umeme ambapo pamoja na mitaa hiyo itanufaika.
![](https://www.mzawa.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/IMG-20250205-WA0087-1024x682.webp)