NA.MWANDISHI WETU
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Mhe. George Simbachawene ametoa wito kwa jamii kuwekeza Dodoma kwa kuzingatia fursa zilizopo ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za kuuendeleza Jiji hilo.
Ametoa kauli hiyo hii leo OKtoba 24, 2022.wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria ilipotembelea na kujionea maendeleo ya ujenzi wa Mji wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma.
Akieleza majukumu ya Ofisi ya Waziri Mkuu Waziri Simbachawene amesema ofisi yake inajukumu la kuratibu na kusimamia mradi wa ujenzi wa Majengo ya Wizara na Taasisi zake hivyo atahakikisha ujenzi huo unasimamiwa kwa weledi na kukamilika kwa wakati.
“Hadi sasa ujenzi umefika asilimia 50 hadi 80 kwa baadhi ya majengo na kwa upande wa miundombinu ya barabara, nishati, maji na mawassiliano ipo vizuri hivyo nitoe rai kwa wananchi kutumia fursa zilizopo ili kuwekeza Dodoma,” alisema Waziri Simbachawene.
Aliongezea kuwa Uwepo wa mji wa Serikali itasaidia kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi kwa wepesi zaidi.
“Mji huu ndiyo utafanikisha na kurahisisha shughuli za Serikali kwa urahisi kwani kila wizara itakuwa hapa na itafikika kwa wepesi, na niwakaribiahe wananchi kuja kupata huduma mahali hapa”, alisema
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati hiyo Dkt. Joseph Mhagama aliipongeza Serikali ya Awamu wa Sita kwa namna inavyowezesha ujenzi wa Mji wa Serikali kwenda kwa kasi na hii inafaa kuungwa mkono.
“Ninampongeza Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa mstari wa mbele katika kuendeleza Mji huu, na Kamati imeridhishwa na maendeleo ya ujenzi hivyo ninawapongeza ofisi ya Waziri Mkuu kwa kufanya kazi kwa weledi,”alisema Dkt. Mhagama
Akitoa neno mjumbe wa kamati hiyo Mhe. Asha Abdallah ametoa kongole kwa kazi kubwa inayofanywa na serikali huku akiwaasa watanzania kutumia mji huo katika kupata huduma kwakuwa unafikika kwa wepesi.
“Ofisi hizi kupatikana mahali pamoja ni jambo nyeti litakalopunguza kero kubwa za wananchi kwani wizara zote zitafikika kwa wepesi, jueni kuwa serikali haijawatupa inajali sana,”
Naye Mjumbe wa Kamati hiyo Mhe. Salum Shafi amesema kila mmoja aone umuhimu wa kulinda na kutunza majengo yatakayotumika na kuhakikisha wanakuwa wazalendo.
“Mradi huu ni fedha za walipa kodi, hivyo kila mmoja awe mzalendo katika kutunza na kulinda yaweze kutumika kwa muda mrefu katika ubora wake na kuongeza tija katika shughuli za Serikali ,hakika Dodoma imepambika na mama ameifanya kazi vizuri mama tunakupongeza,” alisisitiza
=MWISHO=