Mara baada ya jiji la Dar es salaam kufanikiwa kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Nishati wa wakuu wa Nchi za Afrika Mkuu wa Mkoa huo Mhe Albert Chalamila ametangaza rasmi kuanza kwa shughuli za biashara kwenye jiji hilo saa 24 ambapo uzinduzi rasmi utafanyika februari 22 mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam leo Januari 30,2025 katika ukumbi wa Hotel ya Johari Rotana, RC Chalamila amesema jiji hilo ni muhimu kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi hivyo februari 22 mwaka Mkoa huo utazindua rasmi mpango shughuli za kibiashara kufanyika saa 24, kwa sasa wanaendelea kufunga taa za kutosha na maandalizi ya kufunga kamera yanaendelea vizuri kwa ajili ya usalama
Aidha akizungumzia Mkutano wa Nishati wa wakuu wa Nchi za Afrika RC Chalamila amewashukuru na kuwapongeza wananchi wa Mkoa huo kwa ushirikiano mkubwa walioutoa ikiwemo kuimarisha amani, utulivu na usafi hivvyo ameelekeza wilaya zote kuendelea kusimamia suala la usafi ili Mkoa uendelee kuwa kivutio huku akisisitiza kuwa Serikali inakusudia kuanza kutumia usafiri wa treni na majini kuimarisha usafiri ndani ya jiji hilo.
Vilevile akizungumzia suala la ujenzi wa soko la Kariakoo Chalamila amesema zaidi ya bilioni 28 zimetolewa na Rais Dokta Samia Suluhu kwa ajili ya ujenzi wa soko hilo na kwamba ujenzi wake umefikia asilimia 97 pia amesema kwa sasa bodaboda na bajaji hazijazuiliwa kuingia katikati ya jiji kwani walizuiwa kwa siku chache kutokana na ugeni wa marais wa Afrika.
Sanjari na hilo kwa upande wa Mwenyekiti wa bodi ya soko la kariakoo Hawa Ghasia amesema kuanzia januari 31 wanaanza kuweka majina ya wafanyabiaahara ambao walikuwepo kwenye soko la kariakoo kabla halijaungua ili wasajiliwe na kwamba baada ya hapo watasajili wafanyabiashara wapya na waliokuwa wanadaiwa wanapaswa kulipa madeni yao.