Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Nyang’hwale imepongeza utekelezaji wa miradi ya maendeleo kupitia ilani ya CCM yenye thamani ya zaidi ya Shilingi Milioni 900. Miradi hii inahusisha ujenzi wa mabweni ya wanafunzi, nyumba za watumishi, na usimamizi thabiti ambao umehakikisha ubora wa miradi hiyo uko juu.
Akizungumza wakati wa ziara ya kutembelea na kukagua miradi hiyo, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Nyang’hwale, Alhaji Adam Mtole, alisema wameridhishwa na kasi ya utekelezaji wa miradi hiyo. Aliongeza kuwa hatua hiyo ni ushahidi wa juhudi kubwa za Rais Samia Suluhu Hassan kuhakikisha watoto wanasoma katika mazingira bora na kuwepo makazi salama kwa watumishi wa umma.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale, Grace Kingalame, alisema serikali imefanya kazi kubwa kuhakikisha miradi yote inasimamiwa kwa umakini na kukidhi viwango vya ubora na thamani ya fedha zilizotolewa.
Wakati wakisoma taarifa za utekelezaji wa miradi hiyo, Mtendaji wa Kijiji cha Lyilu, Sekelwa Dotto, na Mkuu wa Shule ya Sekondari Nyamakamba, Mashauli Kasobi, walielezea mafanikio ya miradi ya ujenzi wa mabweni, madarasa, na nyumba za walimu.
Miradi hii imeelezwa kuwa ni sehemu ya jitihada za serikali za kuboresha huduma za kijamii na kuinua kiwango cha elimu wilayani Nyang’hwale.