Na Shomari Binda
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo ” CHADEMA “Wilaya ya Butiama wamepongeza ushindi wa Tundu Lissu kwenye uchaguzi wa chama hicho.
Akizungumza na Mzawa Blog mara baada ya kutangazwa kwa matokeo kwenye ukumbi wa Mlimani City Mwenyekiti wa chama hicho Wilaya ya Butiama Michael Makenji amesema agizo alilotumwa amelikamilisha.
Amesema wanapongeza ushindi alioupata Tundu Lissu akiamini lengo la kukivusha chama hicho litafanikiwa
Makenji amesema Lissu anayo nia thabiti ya mabadiliko ikiwa ni pamoja na kufanya vizuri kwenye uchaguzi ikiwa ni pamoja na kushika dola.
Amesema wanachama wa Chadema Wilaya ya Butiama walitangaza mapema kumuunga mkono Lissu wakiamini katika maono yake.
“Tunapongeza ushindi alioupata mgombea tuliyekuwa tukimuunga mkono mheshimiwa Tundu Lissu tukiamini atakivusha chama chetu.
“Wanachama Wilaya ya Butiama wanapongeza ushindi alioupata Tundu Lissu na kuwaomba wanachama wote kuwa wamoja baada ya uchaguzi “, amesema.
Freeman Mbowe akizungumza mara baada ya matokeo kutangazwa amesema moyo wake umeridhika na matokeo na kuomba viongozi waliochaguliwa kukijenga chama kwa kuanzia pale walipoishia na kudai demokrasi imetumika.
Kwa upande wake Tundu Lissu amewashukuru wajumbe kwa kuonyesha imani kwake na kuahidi kufanya kazi za chama kwa kushirikiana na kila mmoja.
Katika matokeo ya nafasi ya Mwenyekiti wa Chadema Taifa Tundu Lissu amechaguliwa kwa kupata kura 513 dhidi ya Freeman Mbowe aliyepata kura 482 kati ya kura 996 zilizopigwa
John Heche amechaguliwa kwenye nafasi ya Makamu Mwenyekiti Bara akipata kura 577 dhidi ya mpinzani wake wa karibu Ezekiel Wenje aliyepata kura 372 na Said Mzee Said akichaguliwa Makamu Mwenyekiti Zanzibar.