Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango, amewahimiza Watanzania wote kufichua vitendo vya ukatili ili hatua stahiki zichukuliwe dhidi ya wahusika. Wito huo umetolewa leo, tarehe 20 Januari 2025, katika Maadhimisho ya Miaka 25 ya Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA), yaliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC), ambapo alihudhuria akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Makamu wa Rais alibainisha kuwa wanawake, watoto, na wanaume wengi hukumbwa na ukatili wa kijinsia au kimwili lakini hawaripoti matukio hayo kwenye vyombo vya sheria. Aliongeza kuwa baadhi ya mila na desturi potofu zimekuwa zikikandamiza waathirika wa ukatili huo.
Mhe. Mpango alieleza kuwa, licha ya juhudi za Serikali katika kuhakikisha usawa wa kijinsia, bado wanawake ambao ni zaidi ya nusu ya idadi ya watu nchini wanakumbana na changamoto za kubaguliwa na kukosa haki ya kumiliki mali. Alisisitiza kuwa kwa mujibu wa Mpango wa Kitaifa wa Kupinga Vitendo vya Kikatili dhidi ya Wanawake wa mwaka 2016, asilimia 40 ya wanawake wamepitia ukatili wa kimwili, huku asilimia 20 wakikumbana na ukatili wa kingono, baadhi yao wakiwa na umri wa chini ya miaka 15.
Kwa mujibu wa Ripoti ya UN Women Social Institution and Gender Index (SIGI) ya mwaka 2022, ukatili wa kijinsia nchini Tanzania unaendelea kujitokeza kupitia ndoa za utotoni, ubaguzi ndani ya familia, ukosefu wa uhuru wa kupanga uzazi, na changamoto za umiliki wa ardhi. Ripoti ya Benki ya Dunia ya mwaka 2022 inaonyesha kuwa asilimia 40 ya wanawake wenye umri wa miaka 15-49 wamepitia ukatili wa kimwili, huku asilimia 17 wakikumbana na ukatili wa kingono.
Makamu wa Rais alieleza kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imechukua hatua madhubuti kuhakikisha usawa wa kijinsia kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, pamoja na mipango kama Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025, Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano, na Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia ya mwaka 2000.
Aidha, alitaja kuwa Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imepiga hatua kubwa katika kuhakikisha usawa wa kijinsia kwenye ngazi za uongozi wa Mahakama. Kwa mfano, asilimia 33 ya Majaji wa Mahakama ya Rufani, asilimia 38 ya Majaji wa Mahakama Kuu, na asilimia 50 ya Mahakimu wa Mahakama za Hakimu Mkazi ni wanawake.
Mhe. Mpango alisisitiza umuhimu wa jamii kusherehekea mafanikio ya wanawake ili kuwahamasisha wasichana na wanawake wengine. Alitoa mifano ya wanawake mashuhuri nchini kama Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa kwanza mwanamke wa Tanzania, na Bibi Titi Mohamed, mwanaharakati wa kupigania uhuru wa Tanzania.
Pia, aliwahimiza Majaji na Mahakimu wanawake nchini kuhakikisha wanajiunga na kuhuisha uanachama wao wa TAWJA kwa kulipa ada ili kuimarisha mshikamano wa chama hicho.
Kwa upande wake, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, aliishukuru Serikali kwa kuongeza idadi ya Majaji wa Mahakama ya Rufani kutoka 17 mwaka 2021 hadi 40 mwaka 2025. Alisisitiza jukumu la Majaji na Mahakimu kutumia Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 kufanikisha malengo ya kijinsia na kisheria.
Mwenyekiti wa TAWJA, Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Barke Sehel, alisema mafanikio ya chama hicho kwa miaka 25 yametokana na ushirikiano mzuri kati ya Serikali na Mahakama. Chama cha TAWJA, kilichoanzishwa mwaka 2000, kiliadhimisha Jubilei ya Miaka 25 kwa kaulimbiu: “Jubilei ya Miaka 25 ya TAWJA: Kusherehekea Utofauti na Mshikamano katika Usawa wa Kijinsia.”