Mwenyekiti Mstaafu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa na Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, leo, Januari 19, 2025, amewataka wanachama wa CCM kutobweteka, akisisitiza kuwa kila wakati wanapaswa kufahamu kwamba uchaguzi ni mgumu. Alisema, “Falsafa ya jeshi ni kwamba vita vitakuwa vigumu,” hivyo maandalizi ya chama lazima yawe ya kiwango cha juu, kama maandalizi ya vita.
Akizungumza katika Mkutano Mkuu Maalum wa CCM mjini Dodoma, ulioongozwa na Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, Mhe. Kikwete alisema, “Maandalizi yetu yanapaswa kuwa ya hali ya juu, kwani tunakwenda kwenye vita kubwa.” Alisisitiza kuwa viongozi waende kwa wananchi na wanachama wa CCM kuwaeleza hatua zinazochukuliwa na kile kilichofanyika hadi sasa.
Aidha, alisema kuwa maelezo yaliyotolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yamedhibitisha kuwa, “Kuwepo kwenu ninyi hatukukosea. Ninyi ni watu makini, mnajua mnachokifanya na mnajua kinachotakiwa kufanyika. Kwa haya mliyoeleza hapa, ushindi wa CCM ni dhahiri.“
Hata hivyo, Mhe. Kikwete ameonyesha hekima ya hali ya juu na uzoefu mkubwa katika siasa kwa kutoa ushauri thabiti unaolenga kuimarisha umoja na uwazi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Mhe. Kikwete amesisitiza umuhimu wa kufuata utaratibu rasmi wa chama kwa kupitisha azimio la kuidhinisha majina ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi, kama wagombea wa urais wa mwaka 2025.
Katika hotuba yake, Kikwete amepongeza kazi kubwa iliyofanywa na viongozi hao, akibainisha kuwa ushindi wa CCM katika uchaguzi mkuu ujao hauna shaka kutokana na mafanikio yaliyopatikana.
“Kama tumekubaliana katika mkutano huu, basi Rais Samia na Rais Mwinyi wanaelekea kushinda tena kwa kipindi kingine cha miaka mitano. Lakini ni muhimu tupitishe azimio rasmi ili kuhakikisha tunazingatia taratibu za chama na kutoa ujumbe wa mshikamano kwa wanachama wote,” alisema Kikwete.
Kwa kuhitimisha, Kikwete aliwatia hamasa wajumbe kwa kuanzisha wimbo wa kuonyesha imani kwa Rais Dk. Samia na Dk. Mwinyi, hatua iliyosababisha shangwe kubwa ndani ya ukumbi wa mkutano.
Hatua hii ya Rais Mstaafu Kikwete imeonyesha uzalendo na umakini wake katika kulinda mshikamano wa CCM, huku akisisitiza umuhimu wa kuheshimu misingi ya chama.