Kanisa la Assemblies of God Gospel Church International (AGGCI) kupitia ibada maalum limewakumbuka watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu kwa kuwapatia misaada mbalimbali.
Askofu wa kanisa hilo, Dkt. Robert Ngai, wakati wa ibada hiyo iliyofanyika katika kanisa hilo lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Geita, aliwataka waumini na jamii kwa ujumla kuwa na moyo wa huruma na kuwasaidia watoto wasiojiweza pamoja na wale wanaolelewa kwenye vituo maalum.
“Ibada iliyo njema na inayompendeza Mungu ni pamoja na kuwasaidia watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu. Huu ni wito wa kila mmoja wetu kuwa na mguso wa upendo kwa wahitaji hawa.” Alisema Dr. Robert Ngai – Askofu wa Kanisa la AGGCI.
Katika mahubiri yake, Askofu Ngai pia aliwahimiza waumini kuwa waaminifu katika maisha yao ya kila siku, akisisitiza kuwa uaminifu ni moja ya misingi inayojenga jamii iliyo thabiti.
“Ni lazima tuwe waaminifu. Uaminifu siyo tu tunapoonekana, bali ni tunapokuwa peke yetu na katika kila jambo tunalofanya.”Alisema  Dr. Robert Ngai – Askofu wa Kanisa la AGGCI
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kituo cha Kulelea Watoto cha Bright Light, Bw. Methew Daniel, alielezea changamoto zinazowakabili kituo hicho, zikiwemo upungufu wa chakula na gharama za matibabu kwa watoto.
Miongoni mwa waumini walioshiriki ibada hiyo, Bw. Gwamwaka Mwamgongwa aliwataka watu binafsi na taasisi kushirikiana kwa ukarimu katika kuboresha maisha ya watoto hawa.