Na Saidi Ibada, Morogoro
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Dr Selemani Jafo amesema jukumu la kuhakikisha mazingira yanakuwa salama na rafiki kwa kila kiumbe ni suala la kila mtu kwani maisha ya mwanadamu kwa kiasi kikubwa yanategemea mazingira.
Hayo ameyasema wakati wa maandamano ya amani ya kupinga uchomaji moto milima na uchafuzi wa mazingira Mkoani Morogoro, tukio ambalo limehitimishwa kwa zoezi la upandaji wa miti ya matunda takribani 100 katika Shule ya Sekondari Kilakala, iliyopo Manispaa ya Morogoro.
Waziri Jafo amesema kuwa Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine wa mazingira wataendelea kutoa elimu kwa Wananchi kuhusu umuhimu wa utunzaji wa mazingira ili kuepukana na uchomaji moto milima hususani safu ya milima ya uluguru.
“Niwaombe wananchi mtambue kwamba ninyi ndio watu muhimu kuhakikisha mazingira yanakuwa salama, kabla ya kuchafua mazingira mfikirie yule atakayeathirika na uchafuzi huo. Hivyo niwasihi kuwa muendelee kuweka salama mazingira kwani uhai wetu unategemea mazingira, pandeni miti ya matunda kwa wingi na mnapofanya shughuli zenu za mashamba msiunguze misitu kwani kwa kufanya hivyo mnakausha vyanzo vya maji”, Jafo
Aidha, Waziri Jafo amewataka viongozi wa mitaa na kata kuwa mstari wa mbele kuhimiza utunzaji wa mazingira na kuwachukulia hatua stahiki wote wanaokiuka kwa makusudi kanuni za mazingira hasa wakazi waishio pembezoni mwa milima ya uluguru kujiepusha na uchomaji wa milima.
“Viongozi kazi yenu ni kuhakikisha mazingira katika maeneo yenu yanakuwa katika hali ya usafi, muwahimize watu wapande miti kwa wingi na pale ambapo mnaona mtu anakengeuka msisite kumchukulia hatua stahiki”, amesema Waziri Jafo.
Akizungumzia katika tukio hilo Balozi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais, Chage Alex Chage amezishukuru taasisi binafsi zinazojishughulisha na utunzaji kwa kazi wanazofanya ya kuhakikisha mazingira yanakuwa katika hali ya usafi wakati wote.
“Nawashukuru wadau na taasisi za mazingira kwa kazi mnazozifanya ya utunzaji wa mazingira, hili sio jukumu la serikali peke yake badala yake kila mmoja kwa nafasi yake aepukane na uchafuzi wa mazingir, huko mlipo mkawe mabalozi wazuri wa mazingira”, amesema Balozi Chage.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Kilakala, Mhe. Marco Kanga amesema ujio wa Waziri katika kata yake unaenda kuongeza morali ya wananchi katika suala la utunzaji wa mazingira ambapo amebainisha kuwa wanaenda kuandaa kampeni ya kupanda miti 5 ya matunda kwa kila kaya.