Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa amesema takwimu za mwaka 2021 zinaonesha kuwa watalii wanaokuja nchini Tanzania wameongezeka kwa asilimia 48.6 kutoka watalii 620,867 mwaka 2020 na kufikia watalii 922,692 mwaka 2021.
Mheshimiwa Majaliwa amesema mbali na kuongezeka kwa idadi ya watalii nchini, pia mapato yatokanayo na utalii yameongezeka kwa asilimia 81.8 kutoka Dola za Marekani milioni 714.59 mwaka 2020 na kufikia Dola za Marekani bilioni 1.3 mwaka 2021.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumatano, Oktoba 5, 2022) alipomuwakilisha Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwenye ufunguzi wa Mkutano wa 65 wa Shirika la Utalii Duniani – Kamisheni ya Afrika unaofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Gran Melia Jijini Arusha.
“Pia takwimu za mwaka 2022 zinaonesha kuwa Sekta ya Utalii inazidi kuimarika zaidi hususan baada ya uzinduzi wa Programu Maalumu iliyotekelezwa na Mheshimiwa Rais Samia ya The Roya Tour iliyozinduliwa rasmi Aprili 2022 katika soko letu la utalii la kimkakati nchini Marekani.”
Amesema kuwa mafanikio hayo ni matokeo ya mwongozo mzuri uliotolewa na Shirika la Utalii Duniani kwa nchi wanachama ikiwemo Tanzania katika kukabiliana na athari za UVIKO – 19. “Kwa msingi huo, ninatumia fursa hii kulishukuru Shirika la Utalii Duniani hususan, kwako Mheshimiwa Zurab Pololikashvili, Katibu Mkuu wa Shirika la Utalii Duniani kwa kuiongoza vema sekta ya utalii katika kipindi chote cha janga hilo.”
Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema lengo la Serikali ni kuendelea kuongeza idadi ya watalii wanaoingia nchini hadi kufikia watalii milioni tano na mapato ya Dola za Marekani bilioni sita ifikapo mwaka 2025.”Utajiri wa vivutio vya utalii tulivyonavyo umeifanya sekta ya utalii kuwa muhimili muhimu wa uchumi wa nchi yetu.”
Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kutoa rai kwa mashirika na taasisi za kimataifa kuendelea kuiamini Tanzania na kuichagua kama sehemu sahihi ya kufanyia shughuli mbalimbali ikiwemo mikutano adhimu kama hii.