Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, amesema Chama kimeona umuhimu wa kuwajengea uwezo viongozi wote wapya ndani ya Chama na kwamba baada ya Kukamilika kwa Uchaguzi unaondelea kote nchini watapatiwa mafunzo ili watekeleze majukumu yao kwa ufanisi.
Aidha, amesema CCM bado ni eneo muhimu katika kuzalisha viongozi bora na tegemeo kwa maendeleo ya nchi ndio maana kimeendelea kuaminiwa na watanzania katika kushika hatamu ya kuliongoza Taifa.
Shaka ameyasema hayo aliposhiriki mkutano mkuu wa uchaguzi wa viongozi wa CCM Wilaya ya Dimani, Mkoa wa Magharibi kichama ambao umefanyika leo Oktoba 2, 2022, Kiembesamaki.
Asema viongozi wanapaswa kufanya kazi kwa kuzingatia mipaka kulingana na Katiba ya CCM, kanuni na miongozo ya Chama, hivyo ni lazima kujengewa uwezo kuanzia ngazi ya shina hadi Taifa ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ndugu Samia Suluhu Hassan katika hatua ya kujiimarisha.
“Wengi tuliopo hapa ni viongozi wapya, tumekabidhiwa dhamana hii muhimu ya uongozi, Chama kimeweka mpango maalumu, kama alivyoelekeza Mwenyekiti wetu Samia Suluhu Hassan ndani ya muda mfupi ujao wa kuwapatia mafunzo elekezi viongozi katika ngazi zote ili muweze kumudu vyema kazi zenu,” amesema Shaka.