Na: Mwandishi Wetu – Dodoma
Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu Prof. Jamal Katundu amefungua kikao kazi cha wadau kwa lengo la kupitia, kutoa maoni na kuthibitisha rasimu ya Mwongozo, viwango sanifu na mfumo wa utekelezaji wa Programu ya Stadi za Maisha kwa vijana nje ya shule.
Profesa Jamal amesema hayo jijini Dodoma alipokuwa akifungua kikao kazi hicho na kueleza kuwa, Ofisi ya Waziri Mkuu ilianza kufanya mapitio ya Mwongozo wa Stadi za Maisha wa mwaka 2009 kwa lengo la kuhakikisha masuala mapya yanayojitokeza katika duru za kimataifa, kikanda na kitaifa kwa ajili ya maendeleo ya vijana yanahuishwa kwenye mwongozo huo.
“Stadi za Maisha ni elimu, mbinu na maarifa ambayo hutolewa kwa vijana kwa lengo la kuhamasisha mabadiliko chanya ya tabia, hivyo utekelezaji wa mwongozo huu utasaidia kutengeneza afua madhubuti zitakazo wawezesha vijana kushughulikia changamoto nyingi zinazowakumba,” amesema
Amefafanua kuwa, Serikali kupitia wizara yenye dhamana na maendeleo ya vijana iliona umuhimu wa kuwa na mwongozo huo kwa kuweka mfumo wa uratibu, ufuatiliaji, tathmini na taarifa za utekelezaji ili kusaidia kwa kiasi kikubwa kufanikisha utekelezaji wa programu hiyo ya stadi za Maisha kwa vijana nje ya shule.
Sambamba na hayo, Prof. Jamal Katundu ameshukuru Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu Duniani (UNFPA) kwa ushirikiano na Serikali katika kufanikisha utekelezaji wa programu za maisha kwa vijana hapa nchini.
Kikao kazi hicho kitafanyika kwa siku mbili kuanzia tarehe 29 hadi 30 Septemba, 2022 ambapo wadau hao watapitia nyaraka mbalimbali ikihusisha Mwongozo na Viwango sanifu vya utoaji wa elimu ya stadi za maisha pamoja na mfumo wa uratibu, ufuatiliaji, tathmini na taarifa za utekelezaji wa programu hiyo.
MWISHO