Home Biashara NMB YASHINDA TENA TUZO YA BENKI BORA WATEJA BINAFSI TANZANIA

NMB YASHINDA TENA TUZO YA BENKI BORA WATEJA BINAFSI TANZANIA

Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa benki ya NMB, Filbert Mponzi (katikati), Meneja Mwandamizi wa Mahusiano ya Serikali wa Benki ya NMB – Amanda Feruzi (kulia) na Meneja Mwandamizi wa Mahusianao ya Biashara ya Nje ya Nchi wa Benki ya Nmb – Lucy Kimei (kushoto) wakifurahia tuzo ya Benki Bora ya Wateja Binafsi na Biashara Tanzania kwa mwaka 2022 kutoka jarida la Global Banking and Finance Mara baada ya Hafla ya Ugawaji Tuzo uliofanyika jijini London nchini Uingereza hivi karibuni.

Na Mwandishi Wetu
Kwa mwaka wa pili mfululizo, Benki ya NMB imeshinda tuzo ya benki kiongozi ya kuwahudumia wateja binafsi nchini kutokana na ubora wa huduma zake kukidhi mahitaji ya huduma za kifedha za umma wa walio wengi.
NMB ilitunukiwa tuzo ya Benki Bora ya Wateja Binafsi Tanzania kwa mwaka 2022 kwenye hafla ya tuzo za Global Banking and Finance (GBAF) Awards zilizofanyika huko London, Uingereza.


Tuzo hizo zilianzishwa mwaka 2011 na jarida la Global Banking & Finance Review lenye wasomaji zaidi ya milioni tatu ulimwenguni kote na ambalo shughuli yake kubwa ni kuangazia matukio na maendeleo ya kifedha duniani.


Akizungumza kwenye hafla ya kuwazawadia washindi wa tuzo za mwaka huu, Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa NMB, Bw Filbert Mponzi, alisema ushindi wa benki hiyo ni kutambuliwa kwa dhamira yake thabiti ya kuwawezesha wateja na kulihudumia kikamilifu taifa kwa ujumla.
“Kwetu sisi NMB, mteja na huduma jumuishi za fedha ndiyo msingi wa shughuli zetu zote. Tunatoa huduma nafuu za kifedha kwa wateja zaidi ya milioni tano Tanzania nzima,” Bw Mponzi alibainisha kwenye hotuba yake ya kukubali tuzo hiyo.

Tunawahudumia wateja binafsi wa aina mbalimbali wakiwemo wakulima wadogo, watumishi wa umma, wafanyakazi wa sekta binafsi na wajasiriamali wa kada zote kuanzia ile ya chini kabisa hadi wale wa kati. Kwenye hilo hatuna mpinzani. Tupo kwa asilimia 100 katika wilaya zote nchini,” Bw Mponzi alisema.

Aidha, aliwaambia waliohudhulia hafla hiyo kuwa NMB inaongoza kwa kuwa na mtandao mpana wa usambazaji huduma wenye matawi 227 ambayo asilimia 70 yake yapo maeneo ya vijijini, na zaidi ya NMB Wakala 15,000 pamoja na zaidi ya mashine za kutolea pesa 750.

Pia Bw Mponzi alisema NMB imekuwa ni kinara wa maendeleo ya kidijitali nchini huku akibainisha maeneo kadhaa ambayo benki hiyo imeyaanzisha ikiwemo kuwa benki ya kwanza Tanzania kuwa na mawakala wanaotumia simu za mkononi.

Vile vile NMB imekuwa benki ya kwanza nchini kuwakopesha wateja wake kidijitali na benki ya kwanza kuwawezesha wajasiriamali kuwa na uwezo wa kukubali malipo ya kidijitali kwa njia ya msimbo wa QR.

Dira na mkakati wetu wa sasa hivi na siku zijazo ni kuendelea kutumia maendeleo ya teknolojia za kidijitali kutuwezesha kulisukuma gurudumu la huduma jumuishi za kifedha kwa kutoa huduma zinazohimilika, rahisi na zinazofikiwa na wengi kwa wepesi,” kiongozi huyo alifafanua.

Alisema mafanikio makubwa iliyonayo NMB yasingewezekana bila mchango na msaada wa Serikali na Benki Kuu ya Tanzania ambazo alisema zimesaidia benki hiyo kustawi na kushamili kwa kuweka mazingira wezeshi na rafiki ya biashara na shughuli za kibenki.

Bw Mponzi pia alibainisha kuwa mipango na ushirikiano wa benki hiyo na wadau wake wote umeiwezesha kuwa na matokeo chanya kwenye jamii na kupelekea kuaminika sokoni. Hali hii imepelekea kukua kwa amana za wateja kwa asilimia 24 hadi TZS trilioni 6.5 mwaka 2021.

Kwa mujibu wa Bw Mponzi, tuzo hii ni uthibitisho wa umakini, ari na dhamira ya wafanyakazi zaidi ya 3,500 wa NMB kuhakikisha kuwa benki hiyo sio tu ni Benki Bora ya Wateja Tanzania, bali pia ni benki bora kuliko zote nchini.

MWISHO…

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!