Home Kitaifa MAJALIWA: VIASHIRIA VYOTE VYA UVUNJIFU WA AMANI VIDHIBITIWE

MAJALIWA: VIASHIRIA VYOTE VYA UVUNJIFU WA AMANI VIDHIBITIWE

Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa amewataka watendaji wote Serikalini kuweka mkakati wa kudhibiti viashiria vyote vya uvunjifu wa amani katika maeneo yao.

Mheshimiwa Majaliwa amesema lengo la agizo ni kusisitiza utekelezwaji wa maono na dhamira ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha nchi inaendelea kuwa katika hali ya utulivu ili kuendelea kufikisha maendeleo katika kila eneo.

Amesema hayo leo (Jumatano, Septemba 21, 2022) wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Amani yayofanyika katika ukumbi ya Kuringe, Moshi Kilimanjaro.

Hatuna budi kuitunza amani yetu kulingana na umuhimu wake kwani amani ni tunda la upendo, utulivu, mshikamano na maridhiano.”

Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali ya Tanzania itaendelea kuunga mkono juhudi za kikanda na kimataifa katika kutafuta na kudumisha amani na usalama.

Jukumu la kudumisha amani na kuilinda amani ni ajenda ya kidunia inayomgusa kila mmoja, ili kulinda ustawi wa vizazi vya leo na kesho.”

Pia, amesema kuwa Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan itaendelea kuchukua hatua na tahadhari zote zinazohitajika ili kuendelea kudumisha amani nchini.

Serikali ya Awamu ya Sita, inafanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha amani na usalama vinadumishwa kwa kuweka mikakati mbalimbali ya maendeleo inayolenga kutokomeza umaskini. Umaskini ni chanzo kikubwa cha migogoro sehemu nyingi duniani kwa sababu watu wanagombania kufaidika na rasilimali chache zilizopo.”

Ameongeza kuwa kila palipo na amani, shughuli za kiuchumi na kijamii hufanyika kwa ufanisi mkubwa na hivyo kuchochea maendeleo ya nchi na ustawi wa wananchi kwa ujumla. “Niwasihi wananchi kuendelea kutunza na kuilinda tunu ya amani tuliyojaliwa hapa nchini”

Ni lazima tuendelee kuilinda amani nchini kwetu, Watanzania tuendelee kudhibiti yeyote mwenye nia ya kuiharibu amani yetu. Jukumu la kuilinda amani hii ni agenda yetu sote, tuitekeleze.”

Aidha, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa Umoja wa Mataifa kuendelea kuunga mkono ajenda mbalimbali za maendeleo nchini ili kuhakikisha umaskini haugawanyi jamii bali uwe chachu ya kutafuta njia bora ya kujinasua katika hali hiyo.

Naye, Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa Nchini Tanzania, Zlatan Milisic ameipongeza Tanzania kwa kuendelea kuwa kinara katika kudumisha amani katika nchi za Afrika Mashariki na duniani kwa ujumla.

Aidha, alitoa wito kwa jamii yote nchini kuacha kuchukulia mzaha suala la uwepo wa amani kwani yapo mahusiano ya karibu kati ya amani na maendeleo. “Jamii yenye amani inaweza kuweka mipango yake ya maendeleo vizuri na kuitekeleza kwa ajili ya shughuli za maendeleo”

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu amesema kuwa viongozi wa Mkoa wa Kilimanjaro wataendelea kusimamia utunzaji wa amani tuliyonayo kwani ni tunu muhimu tuliyojaliwa nchini.

Sisi viongozi wa mkoa wa Kilimanjaro tutaendelea kushirikiana na taasisi zote zikiwemo za dini kwani uwepo wa amani ni msingi wa ustawi wa wakazi wa mkoa wa Kilimanjaro na Tanzania kwa ujumla”.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!