Home Kitaifa TMA YATOA TAARIFA UWEPO WA KIMBUNGA “DIKELEDI” KATIKA BAHARI YA HINDI MWAMBAO...

TMA YATOA TAARIFA UWEPO WA KIMBUNGA “DIKELEDI” KATIKA BAHARI YA HINDI MWAMBAO WA PWANI YA MSUMBIJI

Na Mwandishi Wetu-
media Dar es Salaam

MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inatoa taarifa ya uwepo wa kimbunga “DIKELEDI” katika Bahari ya Hindi mwambao wa pwani ya Msumbiji.Mifumo ya hali ya hewa inaonesha kuwa kimbunga hicho kwa sasa kipo katika mwambao wa pwani ya Msumbiji na kinatarajiwa kurejea katika Rasi ya Msumbiji leo Alasiri.

Kwa sasa, kimbunga hicho hakiashirii uwezekano wa kusababisha athari za moja kwa moja hapa nchini.

Hata hivyo, kutokana na ukaribu wa maeneo ambayo kimbunga “DIKELEDI” kipo sambamba na maeneo ya kusini mwa nchi yetu, upo uwezekano mdogo wa matukio ya vipindi vifupi vya mvua kubwa katika maeneo ya Pwani ya kusini hususan katika Mikoa ya Lindi na Mtwara kwa siku ya leo tarehe 14 ya Januari, 2025.

Kwa upande mwingine, vipindi vya upepo mkali na mawimbi makubwa ya Bahari vinatarajiwa kwa maeneo ya ukanda wote wa Pwani ya Bahari ya Hindi na maeneo jirani hususan kati ya leo na kesho (tarehe 14 na15) ya Januari 2025.

Aidha, taarifa ya tahadhari ya uwepo wa vipindi vya upepo mkali na mawimbi makubwa Mamlaka ilianza kutoa kuanzia tarehe 11 Januari, 2025 na hali ya upepo inatarajiwa kuwa shwari kuanzia tarehe 16 Januari, 2025.

USHAURI: Watumiaji wa bahari na wananchi kwa ujumla wanashauriwa kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania pamoja na kupata ushauri na miongozo ya wataalam wa kisekta.

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaendelea kufuatilia mwenendo wa kimbunga hicho na athari zake kwa mifumo ya hali ya hewa hapa nchini na itaendelea kutoa taarifa kila inapobidi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!