Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa wa Njombe imelazimika kugeuza gari kuwa ofisi baada ya kuwafuata Walipakodi katika kijiji cha Ukalawa wilaya ya Njombe vijijini Jimbo la Lupembe umbali wa Km 75.9 kutoka Njombe mjini kwa lengo la kuwapelekea huduma karibu na maeneo yao.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo Afisa Msimamizi wa Kodi mkoa wa Njombe Bw. Prichard Richard Gellejah amesema wamewafikia Walipakodi wapya zaidi ya 200 na kuwafanyia usajili pamoja na kuwapatia TIN namba na Control namba.
Amesema kuwa wakati wa zoezi hilo wametoa elimu ya Mlipakodi kwa wananchi waliofika kuhudumiwa na kuwasisitiza umuhimu wa kulipa kodi kwa hiari kwa maendeleo ya Taifa.
Gellejah amesema maendeleo yaliyopo kijijini hapo ikiwemo huduma za Elimu. Afya na umeme ni matokeo ya kodi hivyo wakiendelea kulipa kodi kwa uaminifu maendeleo yatapelekwa zaidi na Serikali katika maeneo yao.
Ameeleza kuwa walilazimika kutolea huduma kwenye gari baada ya kukosa umeme kwenye ofisi ya kijiji ambako pia hapakuwa na mtandao.
“Kutokana na kutokuwepo kwa mtandao wa internet tulilazimika kutafuta kilima na kuegesha gari hapo na kuanza kutoa huduma ambapo kila mlango wa gari kuanzia mbele ulikuwa na mtumishi mwenye kompyuta mpakato akitoa huduma”
amesema Gellejah.
Amebainisha kuwa wameweza kuwahudumia wananchi wote waliofika katika eneo hilo na kuwa kupitia mkakati huo wa kuwafuata Walipakodi katika maeneo yao wanaamini makusanyo ya kodi ya mkoa wa Njombe yataongezeka.
Gellejah amesema kufanikishwa kwa zoezi hilo ni juhudi zilizowekwa na Meneja wa mkoa wa Njombe Bi. Specioza Owure.
Mwisho