Na OR TAMISEMI
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Innocent Bashungwa amesema katika kipindi cha mwaka mmoja wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan madarakani ameuwezesha Mkoa wa Lindi kupata zaidi ya Sh bilioni 141 kwa ajili ya kupeleka miradi ya maendeleo na kufikisha huduma mbilimbali katika vijiji na vitongoji vya mkoa huo.
Bashungwa ameeleza hayo leo tarehe 29 Juni, 2022 mkoani Lindi katika sherehe ya kumpongeza Mheshimiwa Rais Samia kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuleta maendeleo nchi nzima na kupeleza fedha nyingi za maendeleo katika mkoani.
Amesema fedha zilizopelekwa zimewezesha kutekeleza miradi ya maendeleo na kufikisha huduma mbalimbali vijijini kama huduma za maji, umeme, barabara na miundombinu ya elimu na afya.
Bashungwa amesema Rais Samia kupitia serikali ya awamu ya sita anayoiongoza amedhamilia kuondoa kero na changamoto mbalimbli zinazowakabili Watanzania na kufufua uchumi hasa katika maeneo yaliyo nyuma zaidi.
Aidha, amewaagiza viongozi wa Mkoa wa Lindi na wilaya zake kusimamia fedha za miradi kikamilifu, kukusanya mapato na kuwa wakali kwa mtu yeyote anayejaribu kutumia fedha za umma visivyo au kujenga miradi kwa kiwango kisichoridhisha wala kukubalika.
Bashungwa ametoa wito kwa wananchi kutumia fursa za kazi na biashara zilizopo katika Mkoa wa Lindi kama viwanda, gesi, korosho, kujenga hoteli ambapo kwa sasa mkandarasi ameshakabidhiwa eneo ili kuanza kazi ujenzi bandari.
Pia, amewata Watumishi wa Mkoa wa Lindi kufanya kazi kwa uadilifu, uaminifu na ushirikiano na wananchi, kila mmoja awajibike kwa utaalamu wake, ushauri, usimamizi na utoaji wa taarifa kwa wananchi.
Kwa Upande wake, Mkuu wa Mkoa Lindi, Mhe. Zainab Telack amesema Mkoa Lindi umepokea Sh bilioni 30 kwa ajili ya kuboresha sekta ya elimu na Sh bilioni 23 kwa ajili ya kuboresha miundombinu afya.
Amesema katika uboreshaji wa huduma ya maji Mkoa umepokea Sh bilioni 20 na kwa miundombinu ya barabara zinazosimamiwa na TANROADS zimepewa Sh bilioni 18 na zile za TARURA zimepokelewa Sh bilioni 23.
” Lengo la kukusanyika ni kufikisha pongezi kwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na viongozi wote wa serikali wanaomsaidia kutokana na utendaji madhubuti na usimamizi mzuri unaofanywa kwenye miradi ya maendeleo katika mkoa huo na nchi nzima kwa ujumla.“