Home Kitaifa JESHI LA POLISI DODOMA LAWAKUMBUKA WATOTO WENYE UHITAJI

JESHI LA POLISI DODOMA LAWAKUMBUKA WATOTO WENYE UHITAJI

Na Hamida Ramadhan Dodoma

MKUU wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule amesema licha ya kutokea kwa matukio mfululizo ya vitendo vya ukatili wa kijinsia lakini kwa mujibu wa takwimu kutoka dawati la njinsia matukio hayo yamepungua ukilinganishwa na miaka miwili iliyopita .

Senyamule, amesema hayo Jijini Dodoma wakati akifunga kilele cha maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia kilichofanyika jijii hapa kwa uratibu wa Jeshi la Polisi mkoa pamoja na wadau mbalimbali.

ā€œKuna matukio yametokea hivi karibuni kwenye mkoa wetu ikiwemo lile la baba kumnajisi mtoto wake wa miezi sita hadi kufa yalikuwa ni matukio ambayo yalileta taharuki lakini siyo kwamba mkoa ndiyo unamatukio mengi kiasi hichoā€alisema

Kwa Upande wake Kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma George Katabazi, amesema matukio ya ukatili wa kijinsia bado yapo hivyo ipo haja ya wadau pamoja na serikali kuendelea kushirikiana kukomesha hali hiyo.

ā€œSuala la ukatili ni suala mtambuka hivyo ipo haja kwa kila mmoja wetu kushiriki katika kukomesha hali hiyo na sisi kama jeshi la polisi hatutamfumbia macho mtu yeyote atakaye bainika kufanya vitendo hivyoā€alisema Kamanda Katabazi

Wakati huo huo Jeshi hilo wakishirikiana na wanawake wa Samia mkoa wa Dodoma na kufanya matendo ya Huruma katika kituo cha kulelea watoto wenye mtindio wa ubongo cha Upendo Miyuji.

Akuongea kituoni hapa Mkuu wa Mtandao wa Polisi WanawakeTanzania,Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Eva Stesheni amesema kuwa kitendo hicho ni kielelezo cha umuhimu wa jamii kushirikiana kwa pamoja kusaidia wahitaji.

Akizungumza kwa niaba ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma SACP George Katabazi, Stesheni ameeleza kuwa ni jukumu la kila mmoja katika jamii kusaidia wenye uhitaji, na kwamba Jeshi la Polisi linajivunia kuwa sehemu ya juhudi hizo za kijamii.

” Niwaombe wananchi kuendelea kuwa na moyo wa kusaidiana ili kuboresha maisha ya wale wanaohitaji msaada.

Na kuongeza “Ziara hii inadhihirisha dhamira yetu kama Jeshi la Polisi kuwa sehemu ya jamii na kuchangia kwa njia mbalimbali, ili kusaidia jamii na kuleta tabasamu kwa watu wanaohitaji msaada, “amesema

Amesema katika harakati za kuhamasisha mshikamano na ushirikiano kati ya jamii na taasisi mbalimbali, Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma, kwa kushirikiana na makundi mbalimbali wataendelea kujitoa kwa kufanya misaada ya kihisani kwa wasiojiweza ili kupunguza changamoto wanazokutana nazo .

“Kama Jeshi la Polisi, tunaamini kuwa siyo tu jukumu letu kulinda amani na usalama, bali pia ni wajibu wetu kusaidia jamii, hasa kwa watu walioko katika mazingira magumu,tunajivunia kushirikiana na wanawake na Samia, pamoja na Scouts, katika kuleta mabadiliko chanya kwa wenzetu.”amesisistiza

Naye Mkuu wa dawati la jinsia na watoto Mkoa wa Dodoma, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP)Christer Kayombo ,kituo cha Upendo kimekuwa ni mfano bora wa jinsi huduma za kijamii zinavyoweza kuboresha maisha na kuwa kielelezo cha nguvu ya mshikamano huku Anita wito kwa wanajamii kujitoa kusaidia kwa namna yoyote ile ili kujenga jamii bora na yenye mabadiliko.

“Kutoa ni moyo na sio utajiri, kila mtu ana uwezo wa kujitoa kulingana na hali yake ya maisha,tunahitaji kujitoa ili kusaidia kuboresha maisha ya watu na kuleta tabasamu kwa wale wanaohitaji msaada,kufanya matendo ya huruma ni ibada njema,tunaamini kuwa kama kila mmoja wetu atachangia kwa namna yake, jamii yetu itakuwa na maendeleo endelevu, “amesema ASP Kayombo

Amesisitiza kuwa huduma za kijamii, kama zile zinazotolewa na Kituo cha Upendo, zinahitaji ushirikiano wa karibu kutoka kwa taasisi za kijamii na wananchi kwa ujumla na kwamba ushirikiano wa pamoja unaleta matokeo mazuri, katika kufanikisha malengo ya kuleta mabadiliko chanya kwa walio katika mazingira magumu.

Pia, ASP Kayombo amewahimiza wanawake na vijana kujitoa kwa wale wenye uhitaji,ambapo ameeleza, “Wanawake na vijana ni nguzo muhimu katika jamii,tunahitaji kuwa mstari wa mbele katika kusaidia watu wetu kwa kuwa na moyo wa huruma, tunataka kuona mabadiliko yanayoendelea kwenye jamii kwa manufaa ya jamii Taifa lete, ” ameeleza Kayombo.

Kaimu Msimamizi wa kituo cha Upendo Brother John Mbogo mbali na kufurahishwa na kitendo hicho ameeleza kuwa Kituo hicho kimejikita katika kusaidia jamii kwa kutoa huduma za kijamii kwa watu wenye uhitaji ikiwa ni pamoja na yatima, watu wazima wenye ulemavu, na watoto wa mitaani.

Kwa upande mwingine, Kaimu huyo Msimamizi ameongeza kuwa msaada huo kutoka kwa Jeshi la Polisi unaleta faraja na matumaini kwa watu walio kwenye uhitaji ambapo amesisitiza kuwa msaada wa kijamii kama huo una umuhimu mkubwa katika kujenga jamii yenye mshikamano na huruma.

Amefafanua kuwa kituo hicho kimekuwa ni nguzo muhimu ya kijamii katika kutoa msaada wa kila aina kwa watu walio katika mazingira magumu.

“Leo tumeshuhudia upendo na mshikamano mkubwa kutoka kwa Jeshi la Polisi, Wanawake na Samia, pamoja na Scouts, ambao wameleta msaada mkubwa kwa wahitaji wetu hapa kituoni,kama Kituo cha Upendo, tunajivunia sana kushirikiana nanyi katika juhudi za kuboresha maisha ya watu hawa wenye uhitaji,” amesema Brother Mbogo.

Ameeleza kuwa Kituo cha Upendo Miyuji kimejizatiti kutoa huduma muhimu za kijamii ambazo zinajumuisha chakula, mavazi, elimu, na huduma za kiafya kwa watoto na watu wazima wanaoishi katika mazingira magumu na kwamba Kituo hicho kinawahudumia watu wengi ambao kama wakiishi bila msaada kutoka kwa watu wengine, wangeweza kukosa huduma muhimu za kila siku.

“Kituo chetu kimekuwa na mchango mkubwa katika maisha ya watu wengi hapa Dodoma, tunasaidia watu wenye ulemavu ambao wanahitaji huduma za afya, na watoto wa mitaani ambao wanahitaji makazi na uangalizi, msaada huu unaenda kutupunguzia baadhi ya changamoto zinazowakabili, “amesema na kueleza;

Kwa msaada huu, tunapata nguvu mpya ya kuendelea na huduma zetu,hii inadhihirisha kuwa ushirikiano wa taasisi na watu mbalimbalia unaweza kufanya mabadiliko makubwa katika maisha ya wahitaji,sisi kama Kituo cha Upendo, tunashukuru sana kwa msaada huu, na tunaahidi kuendelea kutoa huduma kwa watu walioko katika mazingira magumu,” amesema Brother Mbogo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!